Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Singida, Evodius Katare, akizungumza kwenye mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi wakishiriki katika mkutano huo.
Mchungaji Dkt. Syprian Hilinti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ((KKKT) Singida akishiriki mjadala kwenye mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi wakishiriki katika mkutano huo.
Mdau wa uchaguzi, Pascal Ntatau akichangia jambo kwenye mkutano huo.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa tahadhari kwa Vyama vya siasa wagombea nafasi mbalimbali za uongozi na wananchi kuwa wajihadhari na vitendo ama matamshi ambayo yanaweza sababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi kuwa watachukuliwa hatua kwani sheria za nchi hazijasimama.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manunuzi na Lojistik wa tume hiyo, Emmanuel Urembo wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi Mkoa wa Singida uliofanyika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa mkoani hapa.
” Wakati Tume inaendelea kuratibu kusimamia na kuendesha uchaguzi huu kwa kutumia sheria za uchaguzi, Vyama vya siasa wagombea na wananchi wanakumbushwa kuwa katika kipindi hiki, sheria nyingine za nchi hazijasimama hivyo wajihadhari na vitendo ama matamshi ambayo yanaweza sababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi.” alisema Urembo.
Alisema Tume inawahakikishia wananchi kuwa imejipanga katika kusimamia uchaguzi wa mwaka huu kwa kufuata Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali na inaamini kuwa kila mdau akitimiza wajibu wake kwa kufuata taratibu Watanzania wataweza kupiga kura kwa amani siku ya uchaguzi.
Urembo alisema Tume inatumia nafasi hii pia kuwatoa hofu wapiga kura wote wenye mahitaji maalumu kwa kuwa maelekezo yametolewa kwa watendaji wa uchaguzi kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu, wajawazito, akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na watoto vituoni, wazee na wagonjwa.
Aliongeza kuwa kwa wale wasiojua kusoma na kuandika wataruhusiwa kwenda na watu wanaowaamini kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
” Kwa watu wenye ulemavu wa kuona kila kituo cha kupigia kura kutakuwa na kifaa cha maandishi ya nukta nundu ‘tactile ballot folder’ hii ni kwa wale wanaofahamu kutumia maandishi hayo na wasioweza wataruhusiwa kwenda kituoni na mtu anayemuamini wa kuweza kumsaidia.” alisema Urembo.
Aidha Urembo alisema kwa wenye ulemavu wa viungo vituturi vitakavyotumika kupiga kura vinaruhusu kuwahudumia kwani kuna pande mbili tofauti, upande mmoja kuna urefu wa kutosha na kikigeuzwa kinakuwa kifupi kumwezesha mwenye ulemavu wa viungo kupiga kura.
Urembo alitumia fursa hiyo kuwaambia kuwa kila mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze na kadi yake ya kupigia kura katika kituo alichojiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi ya kikatiba na kuwa Tume itaendelea kutoa taarifa kwa wakati na kwa njia mbalimbali kuhakikisha wananchi wanafahamu na kuelewa mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.