Mbunge mteule wa viti maalum kupitia vijana, Asia Halamga akizungumza wakati akiomba kura kwa wagombea wa CCM kwa nafasi ya udiwani na urais kwa wananchi wa mtaa wa Nakwa Kata ya Bagara Mkoani Manyara.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba akiomba kura kwa wagombea wa CCM kupitia nafasi ya udiwani na urais kwa wananchi wa mtaa wa Nakwa Kata ya Bagara Mkoani Manyara.
****************************************
Na Mwandishi wetu, Babati
WAKAZI wa Mkoa wa Manyara wameonywa kuwachagua wagombea wa vyama vya upinzani kwani ni wapinga maendeleo hivyo kutambua kuwa wakiwachagua viongozi wa vyama vya upinzani ni sawa na kuionja sumu kwa kuilamba.
Hayo yameelezwa na Mbunge mteule wa viti maalum vijana, Asia Halamga, wakati akiomba kura kwenye kata ya Bagara mjini Babati kwa wagombea wa nafasi za udiwani na urais kupitia CCM.
Halamga ambaye alishinda nafasi hiyo hivi karibuni kupitia Mkoa wa Manyara, awali alishawahi kuwa Katibu wa UVCCM Wilayani Kongwa mkoani Dodoma, diwani wa viti maalum wa Halmashauri hiyo pia Katibu wa UVCCM Mkoani Kilimanjaro na sasa anasubiri kuapishwa Bungeni baada ya uchaguzi mkuu.
Amesema wapinzani wengi huwa wanapinga maendeleo hivyo wananchi wakiwachagua ni sawa na kuonja sumu kwa kuilamba.
Ametoa mfano kwa mwaka huu kwenye bunge la bajeti, baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani walikimbia kwa hofu ya korona na kuwaacha wabunge wa CCM wakapitisha bajeti hiyo.
Amewapa mfano wa mzazi anayemrusha mtoto wake juu huku amefunga taulo kisha likaanguka ghafla mbele ya mama mkwe na kuwapa mtihani wa kuokota taulo au kuokoa mtoto.
“Wana Manyara tunapaswa kumdaka mtoto ambaye ni mgombea urais John Magufuli na wagombea wa CCM kwani wapinzani ni taulo hivyo tusiliokote,” amesema Asia.
Amesema anatarajia kwa mwaka huu wa uchaguzi wananchi wa Manyara hawatafanya makosa kama ya uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo baadhi yao waliwachagua madiwani na wabunge wa wapinzani.
Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Manyara, Mosses Komba amesema kwa mwaka huu kura zitahesabiwa kwa kila wilaya kulingana na asilimia.
Komba amesema kila wilaya itakaguliwa ili kubaini kura ilizotoa kwenye nafasi ya urais hivyo wananchi wa Manyara wasipoteze kura zao.
“Kura za mgombea urais wa CCM John Magufuli zinapaswa kujaa saa mbili asubuhi na siyo vinginevyo hivyo hivyo kwa wagombea wa CCM wa nafasi za ubunge na udiwani,” amesema Komba.