Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela , jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila, akiongoza maombi kwenye kongamano la maombi ya kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu lililofanyika kanisani hapo mwishoni mwa wiki.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Glory Temple Assemblies of God, James Mwaipyana akielezea umuhimu wa kuombea Serikali iliyopo madarakani na vyombo vya ulinzi.
Mchungaji Dkt. William Kopwe ambaye ni Mwenyekiti wa Hudama ya Nyumba ya maombi na Mchungaji wa Kanisa la KKKT akielezea kila mamlaka inatoka kwa Mungu.
Mchungaji wa Huduma ya Maombi Tanzania, .Alice Kopwe akizungumza kwenye Kongamano hilo.
Maombi yakiendelea kwenye kongamano hilo.
Na Dotto Mwaibale.
KANISA la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela , jijini Dar e Salaam kwa kushirikiana na huduma mbalimbali za maombi limefanya kongamano la maombi la kuliombea Taifa liwe na amani wakati huu wa kampeni hadi utakapofanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.
Kongamano hilo liliandaliwa na IGO Africa for Jesus Prayer Movement kwa kushirikiana na Nyumba ya Maombi na Timu ya Maombi Kibaha.
Maombi hayo yaliongozwa na Askofu Kiongozi wa Kanisa hilo na Mkurugezi wa IGO Africa for Jesus Prayer Movement, , Flaston Ndabila kwa ajili kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wakiwepo wachungaji, maaskofu na waumini kutoka jijini Dar es Salaam na mikoani.
Baadhi ya viongozi wa dini waliokuwa wanenaji katika maombi hayo walikuwa ni Bishop Sedrick Ndonde, Bishop James Mwaipyana na Mchungaji Dkt.William Kopwe.
Akifungua kongamano hilo lililofanyika mwishoni mwa wikii, Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali.
Alisema kufuatia kuwepo kwa changamoto hizo, anahitajika mtu au watu wa kuzitatua kwa kuziombea na kuelimisha wagombea.
Ndabila alisema kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa njia iliyonyooka ili viwe na busara ya kufanya uchaguzi bila ya umwagaji damu.
Aliongeza kuwa wao kama kanisa wanamuombea mama Janeth Magufuli Mungu ampe hekima ya kumshauri mumewe azidi kuliongoza taifa letu kwa busara kuepuka umwagikaji wa damu wakati huu wa uchaguzi.
Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuanza kuimba wimbo wa taifa kwenye kampeni zao huku wakimtanguliza Mungu.
Ndabila alisema vita ikitokea wa kulaumiwa litakuwa kanisa kwa sababu halikumuomba Mungu atuepushe na machafuko wakati wa uchaguzi.
“Wagombea wote ni watoto wa kanisa hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu,” alisema Ndabila.
Askofu Ndabila pia aliwaombea kwa Mungu Marais wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu , Masipika pamoja na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli Mungu awape busara na hekima za kumshauri Rais wetu ili aweze kuivusha salama nchi yetu asiwepo mtanzania hata mmoja atakaye mwanga damu.
Ndabila alisema maombi hayo hayaja walenga wagombea pekee bali pia na wapiga kura na watanzania kwa ujumla wao.
Naye Mchungaji Evelyne Mayengo akizungumza kwenye kongamano hilo alimshukuru Mungu kwa kulilinda taifa letu tangu lilipoanzishwa kwa kulifanya taifa lenye umoja na mshikamano ingawa lina makabila mengi.
“Tumshukuru Mungu kwa viongozi wetu wakuu kubadilishana kijiti cha uongozi kwa amani bila kumwaga damu wala kuligawa taifa,” alisema mchungaji huyo.
Aidha, alimshukuru Mungu kuliponya taifa letu na maradhi ya Corona na kutuwezesha kufanya kampeni na uchaguzi mwaka huu.
Mchungaji Alistidia Modest wa Kanisa la MPC akizungumza kwenye kongamano hilo alimshukuru Mungu kwa kuliwezesha taifa letu kuingia kwenye uchumi wa kati kabla ya Mwaka 2025 uliokadiriwa.
Alimshukuru pia Mungu kwa kuifanya nchi yetu kuwa na rasilimali nyingi kama bahari, maziwa, madini yakiwemo ya Tanzanite yanayopatikana nchini mwetu pekee, gesi, milima, mbuga za wanyama na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho.
Naye Mchungaji Alice Kopwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amemuomba Mungu aiwezeshe NEC kusambaza vifaa vya kupigia kura vifike vituoni kwa wakati, vitosheleze na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 28.
Maombi yaliyojiri kwenye kongamano hilo pia yalihusu kuwaombea viongozi wa NEC, vyombo vya dola vitende haki na wote wawe na hofu ya Mungu ili uchaguzi uwe huru na haki.
Kwa upande wake Bishop Sendrick Ndonde aliliombea baraka taifa la tanzania, taifa la Israel na kuwabariki waombaji waliohudhuria katika kongamano hilo ambapo naye Mchungaji Dkt. William Kopwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amemuomba Mungu atupe kiongozi anayetoka kwake.