MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wananchi waichague CCM ili iweze kuwaletea maendeleo.
“Chagueni CCM, chama chenye mipango ya maendeleo na ya kueleweka. Chama chenye mipango ndani ya kitabu chenye kurasa 303. Naomba kura zenu ili tuwaletee maendeleo.”
Alitoa wito huo jana jioni (Alhamisi, Septemba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Misheni.
“Zamani tulikuwa na kitabu kidogo cha kurasa 236 lakini sasa hivi tuna buku kubwa zaidi. Tukitekeleza yote haya, mambo si yatakuwa mazuri zaidi,?” alihoji.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Sumve, Bw. Kasalali Mageni, mgombea udiwani wa kata ya Sumve, Bw. Gervas Kitwala na madiwani wa kata zote za wilaya ya Kwimba.
“Ninaomba kura kwa wapenzi wa vyama vyote, pigeni kura nyingi sana kwa Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge Bw. Kasalali na madiwani wote ili mpate wawakilishi wengi zaidi kupitia viti maalum,” alisema.
Akielezea mafanikio kwenye sekta ya maji wilayani humo, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 2 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Igumangobo, ujenzi wa mradi wa maji Igunguhya na Nyanhiga, upanuzi wa mradi wa maji Kadashi-Nyashana, upanuzi wa mradi wa maji Hungumalwa na upanuzi wa mradi wa maji KASHWASA kwenda kijiji cha Jojiro.
Alisema fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi mingine ya maji ni sh. milioni 118.6 kwa ajili ya miradi ya maji ya uchimbaji wa visima vya Nkalalo na Lyoma na mradi wa uchimbaji wa kisima katika mji wa Sumve.
Kuhusu barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali iliunda TARURA ifuatilie na kukagua maeneo korofi na watoe makaridio ya matengenezo ili zitafutwe fedha za ujenzi. “Malengo ya Serikali ya kuboresha njia za usafirishaji ni pamoja na kuimarisha barabara zote zinazounganisha kijiji na kijiji, kata na kata, wilaya na wilaya ikiwa ni pamoja na madaraja yanayopita kwenye barabara hizo kwa kuyaingiza kwenye mpango ili njia hizo ziweze kupitika,” alisema.