Mratibu wa TASAF Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese akifafanua jambo ofisini kwake
……………………………………………………………………………..
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia kuanza zoezi la uhawilishaji fedha kiasi cha shilingi 299,608,000 kwa walengwa 4,764 wa mpango wa kunusuru kaya masikini waliohakikiwa mwezi Julai 2020.
Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese ofisini kwake leo.
Kasese alisema kuwa zoezi la uhawilishaji fedha katika Halmashauri hiyo litaanza tarehe 23-28 Septemba, 2020. “Malipo ya kwanza katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Mpango wa kunusuru kaya masikini kiasi cha fedha zitakazohaulishwa kwa walengwa 4,764 ni shilingi 299,608,000”. Jumla ya mitaa 70, iliyopo katika Kata 32 itahusika na uhaulishaji huo, aliongeza.
Mratibu huyo alitoa wito kwa walengwa wote kufika katika vituo vyao vya malipo kwa tarehe pangwa kulingana na mitaa yao. “Katika malipo haya, watakaolipwa ni walengwa waliohakikiwa mwezi Julai 2020. Hakuna walengwa kuchukuliana fedha. Kila mlengwa lazima afike mwenyewe na kitambulisho chake. Naamini kila mlengwa atakuwa anatambuliwa na serikali yake ya mtaa na ataliopwa kulingana na kiwango stahiki kilichotumwa kutoka TASAF makao makuu” alisisitiza Kasese.