Bi. Clara Ndyamkana akizungumza na baadhi ya wazazi wa mkoa wa Katavi katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda
Familia moja katika kata ya Makanyagio katika Manispaa ya Mpanda ambayo baba na mama wanaishi mashambani na kuwaacha watoto na bibi yao
…………………………………………………………………………………..
Na. Zillipa Joseph KATAVI
Wazazi wa mkoa wa katavi wametakiwa kuweka waangalizi wa watoto ambao ni watu wazima wenye kujitambua wakati msimu wa kilimo utakapoanza ili kulinda matokeo hasi yanayowapata watoto kufuatia kuachwa wakijilea wenyewe katika msimu huo
Wito huo umetolewa na Bi. Clara Nyamkana ambaye ni Afisa kutoka Dawati la Jinsia la Polisi mkoa wa Katavi wakati akizungumza na wazazi katika kongamano la malezi na makuzi ya mtoto lililofanyika katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi
Bi. Ndamkana amesema kulingana na mazoea wazazi wengi wamekuwa wakiwaacha watoto wakijilea wenyewe msimu wa kilimo unapowadia hali inayopelekea watoto kupata majanga mbalimbali ikiwemo ubakaji
“Watoto wamekuwa wakipitia vitendo vya kikatili katika kipindi cha miezi mitatu hadi mitano na wakati mwingine wanajikuta wakijihusisha na vitendo vya wizi kwa sababu ya kukosa chakula” alisema Ndamkana
Aidha ameitaka jamii kutambua athari zinazowapata watoto pindi wanapokuwa wametendewa vitendo vya ukatili wa kijinsia
Ameongeza kuwa jamii nyingi katika mkoa wa katavi zinaishi katika hali ya umaskini na kutegemea kilimo na kkuonya kuwa hali hiyo isiwe kigezo cha kusababisha familia kutelekezwa
Kwa upande wao baadhi ya wazazi wamekiri kuwaacha watoto na ndugu zao wenye uelewa au wanafunzi wa sekondari kuwalinda wadogo zao
Hata hivyo mmoja wa wazazi hao ambae hakupenda jina lake litajwe amekiri kupata athari baada ya kuwaacha watoto wake watatu wenye umri wa chini ya miaka saba na binti yake wa kidato cha pili
“Nimerudi na mpunga lakini ubwabwa umekuwa mchungu kwangu, binti yangu ana ujauzito wa miezi wa miezi minne! Nimeumia sana halafu aliyempa huo ujauzito ni mtu wa jirani kabisa!” alisema mama huyo
Akizungumzia athari za mimba za utotoni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk. Omary Sukari amesema licha ya kupata matatizo wakati wa kujifungua, wazazi ambao ni watoto mara nyingi hawatoi malezi sahihi kwa watoto wao
Amesema katavi inatajwa kuwa na asilimia 45 ya kuwa na mimba za utotoni
“Kati ya watoto hao asilimia 32 ya watoto wanaozaliwa na watoto hao wamekuwa wakifikishwa hospitali wakiwa na changamoto ya watoto wenye lishe duni” alisema Dk. Sukari