********************************
Na Mwandishi wetu
Wananchi wa Kigoma Mjini mkoani Kigoma wameeleza masikitiko yao juu ya Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia Chama Cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe juu ya kukashifu Ndege zilizonunuliwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kile walichokieleza kiongozi huyo hana nia ya dhati ya kuleta maendeleo kwenye Jimbo la Kigoma Mjini.
Wananchi hao walioonekana katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Kigoma wakiwa na mabango yaliyokuwa na picha ya Mgombea Ubunge wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe ambayo yana maneno yanayoeleza “Mnanunua Ndege za nini?, Zitto Kabwe akishuka kwenye Mtumbwi Mwandiga”
Wakizungumza kwa hisia kali wananchi hao wa Kigoma Mjini, wamesema kwa kipindi ambacho Zitto Kabwe amekuwa Mbunge kwenye jimbo hilo hajafanya shughuli yeyote ya maendeleo zaidi ya maendeleo yaliyofanywa na Rais Dkt. John Magufuli.
“Kiukweli ukiliona hili bango utasema nina mapenzi na huyu bwana (Zitto Kabwe) lakini hajatusaidia chochote kinachohusu maendeleo ya Kigoma Mjini zaidi ya kuponda, nashangaa juzi kaja hapa anasema amekuja Kigoma kwa Ndege hizihizi ambazo ameziponda, na wala hajasema kama zimemuangusha, anadai Ndege ni mbaya lakini yeye ni mtumiaji mkubwa, bora tumchague tu Dkt. Magufuli” alisema Izrael Josephat mkazi wa Kigoma Ujiji
“Kwa kweli Wanasiasa wengine ni wachanga sana leo tunaona Zitto Kabwe anapanda Ndege ambazo alizipinga, safari hii tumesema basi tena hatutamchagua” aliongeza Saidi Mongaa mwenyeji wa Kigoma Ujiji
“Ninasikitishwa na Zitto kwanza anajiita ndugu yetu , ni ndugu gani huyu asiyetutakia mema?, Manispaa yetu inazalisha TZS Bilioni 2 kwa mwaka lakini hii Manispaa haina hata maji, asubiri viongozi wazuri waje ili wamuongoze.” alisema Stephano Chakupewa mkazi wa Kigoma Ujiji.
Akizungumza kuhusiana na Ndege Mgombea Urais wa CCM, Rais Dkt. Magufuli amesema katika kuhakikisha Kigoma inakua na maendeleo amepanga kupanua Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma ili Ndege kubwa (Airbus) ziweze kutua mkoani humo.
“Tunampango wa kupanua Uwanja wa Ndege wa Kigoma, tunataka Ndege kubwa (Airbus) zianze kutua hapa, nimefurahi sana hata wanaopinga Ndege nao wanapanda” amesema Rais Magufuli.
Kwa sasa Rais Magufuli yuko mkoani Kigoma kwa ajili ya kufanya mikutano ya Kampeni na kuomba kura Kwa wananchi baada ya kuwasili mkoani humo na kupokelewa na mamilioni ya wananchi akitokea Biharamulo mkoani Kagera.