Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt. Ayoub Kibao aliyemwakilisha mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam.
Mwakilishi wa Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Ayoub Kibao, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Mkuu wa Idara ya Tiba wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti katika programu ya sikoseli na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Paschal Ruggajo wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza jambo na Dkt. Emmanuel Balandya ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Masomo ya Elimu ya juu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) na Mkuu wa Idara ya Tiba wa MUHAS ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti katika programu ya sikoseli na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Paschal Ruggajo mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam.
Mwakilishi wa Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Ayoub Kibao akizungumza jambo wakati akikagua chumba cha kufanyia kipimo cha kuangalia umeme wa moyo (Electrocardiogram) katika kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam.
********************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
16/09/2020 Kliniki maalum kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa sikoseli ambapo wanaokabiliwa pia na magonjwa ya moyo imeanzishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Pro. Mohamed Janabi amesema wameshirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kupitia Programu yake ya Sikoseli.
Prof. Janabi, amesema juhudi za kuianzisha kliniki hiyo zilianza takribani miaka miwili iliyopita na kwamba inalenga kuboresha huduma za matibabu ya wagonjwa hao.
Amesema JKCI kila wiki huwa tunawaona kwenye kliniki zetu na kwamba kabla ya kuanzisha kliniki hiyo ilimlazimu mgonjwa anayehudhuria kliniki ya sikoseli anayegundulika kuwa na shida ya moyo, kuelekezwa JKCI ili kwenda kupangiwa tarehe ya kuanza kliniki ya moyo.
“Tukaona ni adha kubwa kwao, maana yake analazimika kuhudhuria kliniki mbili. Sikoseli ni ugonjwa wa damu, mtu mwenye sikoseli yupo kwenye uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, japo si wote ambao huishia kupata magonjwa ya moyo, lakini mtu akiwa na ugonjwa wa moyo hawezi kupata sikoseli,” amebainisha.
Ameongeza “Kwa sababu sikoseli wenyewe ni ugonjwa ambao mtu anaupata kwa kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi, uhusiano wake na magonjwa ya moyo ni kwamba sikoseli ni tatizo la kwenye damu, wagonjwa wa sikoseli hukabiliwa na upungufu wa damu, hali hii inaweza kuleta athari kwenye moyo na hata viungo vingine vya mwili.
“Kunapokuwa na upungufu wa damu, maana yake mwili unakuwa na damu chache lakini moyo bado hulazimika kupiga zaidi ili kuisukuma.
“Sasa neno ‘circle’ limetokana na vile visu vya kunolea mpunga (mundu), yaani zile chembe chembe za damu huwa hazipo kwenye muundo wa kawaida wa duara, zinapokuwa kwenye umbo la mundu ‘zina-tendency’ (tabia) ya kugandisha damu.
“Damu inapoganda inaweza kuziba kuziba mishipa ya damu na hali hiyo huwa haichagui itokee wapi, ikiganda kwenye mishipa iliyopo kwenye moyo ndipo uhusiano na magonjwa ya moyo unapotokea, wengne hupata pia ugonjwa wa kiharusi,” amebainisha.
Ameongeza “Zile changamoto zinazotokea kwenye damu ndiyo zinaleta athari kwenye moyo, kwa hiyo sikoseli ndiyo inasababisha ugonjwa wa moyo, lakini mnoyo wenyewe hauwezi kusababisha sikoseli.
“Hivyo, wataalamu tulishauriana na kukubaliana kuanzisha kliniki hii maalum kwa wagonjwa hawa kwa sababu ni magonjwa yanayoingiliana, mgonjwa atakapokuja ataweza kuonwa na madaktari wa magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja,” amesisitiza.
Amebainisha kutokuwa na kliniki ya wagonjwa wa sikoseli kwa upande wa watoto pia watu wazima na kwamba watafanyiwa vipimo vyote vya moyo na damu na kupatiwa dawa kadri itakavyoshauriwa.
“Tumeanza na sikoseli, siku zijazo dhumuni letu ni kufikia hatua ya kuanzisha kliniki moja kwa magonjwa yanayoingiliana kwa mfano moyo na figo, au moyo na kisukari, kumrahisishia mgonjwa kuhudumiwa na kumuepushia adha ya kukimbizana huku na kule, kufuata huduma,” amesema.
Mkuu wa Idara ya Tiba wa Muhas ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti wa Muhas katika programu ya sikoseli na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Paschal Ruggajo amesema kliniki hiyo itawasaidia pia wataalamu kujadiliana na kufanya tafiti zaidi ili kuimarisha na kuboresha tiba za wagonjwa wa sikoseli.
Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Sikoseli Nchini, Arafa Said amepongeza hatua hiyo na kubainisha kwamba gharama za matibabu bado ni changamoto kubwa inayowakabili.
“Wengi wetu hawana bima ya afya na wapo wanaokata tamaa na kuacha kuhudhuria kliniki, tunaendelea kujitahidi kutafuta wafadhili, ili kuwasaidia,” amesema.
Akizungumza, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Ayoub Kibao amewahamasisha watanzania kukata bima ya afya kwani inasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.
“Takwimu zinaonesha nchini kila mwaka watoto 8000 hadi 11,000 huzaliwa na ugonjwa huu, nawashauri hasa vijana wanaotaka kuingia kwenye ndoa, wapime ili kujua iwapo wamebeba vinasaba vya ugonjwa huu ama la,” ameshauri.