Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga akizungumza na Wadau wa Utalii wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kabla ya kuanza kutolewa kwa mafunzo ya usajili wa Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo mkoani Arusha.
Baadhi ya Wadau wa Utalii kati ya 250 wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni walioshiki kutoka katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro wakifuatilia mafunzo ya usajili Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL yanayoendelea kufanyika kwa siku mbili kuanzia leo mkoani Arusha.
Muwezeshaji wa Mafunzo ya usajili Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL, Kelvin Mtei akitoa mafunzo kwa Wadau wanaotoa huduma za Malazi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Mfumo huo wa Kielektoniki utaanza kutumia Oktoba 1, mwaka huu kwa Watoa Huduma hiyo nchini kote
Afisa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Neema Salum akimsajili Juliana Haniu ambaye ni moja Washiriki wa mafunzo ya MNRT PORTAL yaliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha leo.
Muwezeshaji wa Mafunzo ya usajili Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL , Kelvin Mtei akiwasajili baadhi ya Wadau wa malazi walioshiriki mafunzo hayo leo mkoani Arusha.
Afisa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mwinyi Mbegu akimpa maelezo Shabani Hamisi ya namna ya kusajili Wageni wataokuja kulala katika Hoteli yake mara baada ya kupata mafunzo ya kusajili Wageni kwenye MNRT PORTAL yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia jana yaliyomalizika leo Jijini Arusha.
…………………………………………………………………………..
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewatoa hofu Wamiliki wa Huduma za Malazi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa usajili wa Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL utakaoanza kutumika nchini kote Oktoba 1, 2020 umelenga kupata takwimu sahihi za Wageni zitakazosaidia katika kuboresha sekta ya Utalii nchini na si vingunevyo.
Pia, Imesema Usajili huo utalinda siri za Wageni na zitatumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali pekee na sio kwa maslahi binafsi.
Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga alipokuwa akihitimisha mafunzo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili ya usajili Wageni kwenye Mfumo wa MNRT PORTAL kwa Watoa Huduma za Malazi zaidi ya 250 wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara
Amesema Usajili wa Wageni katika Mfumo huo utahusisha Wageni wa ndani pamoja na Wageni kutoka nje ya nchi ambapo lengo kuu ni kupata takwimu zitakazosaidia kuboresha sera, mikakati na mbinu za kukuza utalii nchini.
Amesema Usajili huo mbali ya kusaidia kujua idadi ya Watalii wa ndani bali utawasaidia hata Wamiliki wa malazi hayo kuweka rekodi ya Wageni waliolala katika malazi yao kwa kipindi chote ambacho anafanya biashara hiyo ya malazi.
Chitaunga amesema katika sekta ya utalii mfumo huo umekuwa ukitumika sehemu nyingi Duniani kama vile Uingereza, Marekani na Kanada na si kitu kipya kilichoanzishwa hapa nchini.
Pia amesema mfumo huo utasaidia kurahisisha kazi kwa Wamiliki wa malazi ambapo badala ya kubeba karatasi na kwenda katika ofisi za Wizara ya Maliasili na utalii kwa ajili ya kulipia leseni ataweza kutumia kompyuta yake akiwa ofisini kwake kufanya usajili huo
Mkurugenzi huyo amesema mfumo huo utakaonza kutumiwa na Watoa Huduma za malazi nchini kote mwezi Oktoba 1, 2020 utahusisha hoteli, loji, nyumba za Wageni pamoja na mahema ya watalii.
Ametaja vitambulisho vitakavyotumika katika usajili huo kuwa ni Kitambulisho cha Taifa kwa wageni ambao ni Watanzania na Pasi ya kusafiria kwa Wageni wa kutoka nchi za nje.
Katika hatua nyingine, Chitaunga amesema kuanza kutumika kwa Mfumo huo ni utekelezaji wa takwa la kisheria linalomtaka kila Mmiliki wa Malazi kuanza kusajili Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL.
Mbali na hiyo, Chitaunga amesema matumizi ya mfumo huo utaifanya sekta ya Utalii kwenda katika uchumi wa bluu utakaoiweka Tanzania katika mazigira bora ya kibiashara
Naye Anne Sosteness ambaye ni miongoni mwa Wamiliki wa Malazi katika mkoa wa Arusha aliyeshiriki mafunzo hayo, Amesema mafunzo ni mazuri na ni salama kwa mteja na mtoa huduma kwa ssbabu Mteja anatakiwa kuonesha kitambulisho chaTaifa au pasi ya kusafiria ili aweze kusajiliwa.
Aidha, Amesema mfumo huo unapunguza matumizi ya karatasi ambayo ni rahisi kupotea na kuchanika.