Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Kelema, kata ya Paranga, wilayani Chemba , katika mkutano wa kampeni, Septemba 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Kelema, kata ya Paranga, wilayani Chemba, baada ya kuwasili katika mkutano wa kampeni, Septemba 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*************************************
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inapanga kuanzisha Mamlaka ya Maji Chemba hivi karibuni.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Septemba 13, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Mnadani, Kijiji cha Kelema, Kata ya Paranga, wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kwenye mkutano wa kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge jimbo la Chemba, Mohammed Moni na wagombea udiwani wa CCM.
“Wilaya hii haina mamlaka ya maji. Kwa hiyo tutaanzisha Mamlaka ya Maji ili watumishi wawepo wilayani. Wasimamie kwa karibu na waweze kufuatilia vyanzo vya maji kutokea hapa Chemba wakati tukiendelea kutatua tatizo la maji wilayani hapa. Tutaunda Mamlaka ya maji hivi karibuni.”
Amesema Serikali ilitoa sh. bilioni 1.688 za kutafuta vyanzo vya maji huko Orada, Kisanga, Moi, Mondo na Ndaki. “Pia Serikali ya Awamu ya Tano imetoa sh. milioni 677 za kuchimba visima huko Mondo, Mrijo Juu, Chambalo, Hamai na Chemba.”
“Tuna uhakika tukipata lita za maji za ujazo 4,700 zinatosha kabisa kujenga mtandao wa maji. Kazi ya kuboresha miundombinu ya maji inaendelea. Zimetengwa fedha nyingine, sh. milioni 150 za kusambaza maji Kelema, Msaada na Bumbu.”
Akizungumzia sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa amesema zimetolewa sh. bilioni 1.8 za kujenga hospitali ya wilaya ya Chemba ili wananchi wapate huduma za tiba wakiwa hapohapo badala ya kwenda Kondoa kama ilivyokuwa awali.
“Nia yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hukohuko aliko kwa kuweka zahanati katika kila kijiji, vituo vya afya kwa kila kata. Wakimaliza ujenzi, tumetenga shilingi milioni 500 za vifaa vya hospitali kwa majengo yote saba.”
“Tumepeleka sh. milioni 400 za kituo cha afya kule Hamai, shilingi milioni 500 kule Mrijo na shilingi milioni 400 kule Kwa Mtoro. Kazi ya ujenzi ikiisha, kila kimoja kitapata shilini milioni 250 za vifaa vya tiba.”
Ninawaomba mumpe kura Rais Dkt Magufuli, Mbunge na madiwani wa CCM ili tukamilishe kazi hizi kwa sababu Serikali hii ni ya watekelezaji. Tunasema na tunatenda.”
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Magufuli anataka umeme usambazwe kote nchini na ndiyo maana akaamua kupunguza bei ya kuunganisha umeme.
“Rais wetu kasema anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme. Amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 380,000/- hadi shilingi 27,000/-. Rais wetu kasema ni marufuku kulipia nguzo za umeme. Mwananchi hutakiwi kulipia nguzo yoyote ile. Atakayekuuzia nguzo, mwambie akupe risiti, leta risiti tumlipue huyo Afisa., amesisitiza.
Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na mikutano ya kuomba kura wilayani Kondoa.