Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati na waandishi wa habari.
………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Kiteto
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, inamshikilia Daktari na mtaalamu wa dawa za usingizi kwa tuhuma za kudaiwa kupokea rushwa ya shilingi 180,000 kutoka kwa mzee wa miaka 60 aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume .
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati amesema watumishi hao wawili wa idara ya afya walitaka kiasi hicho cha fedha kwa mzee huyo aliyekuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji wa tezi dume.
Makungu amewataja watuhumiwa hao ni Dokta Martin John Kongora wa hospitali ya wilaya ya Kiteto na mtaalamu wa dawa za usingizi wa hospitali hiyo Fabiano Aweda.
Amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Amesema watuhumiwa hao waliomba rushwa hiyo licha ya mzee huyo kuwa na bima ya afya ya iCHF.
“TAKUKURU Wilayani Kiteto ilipokea malalamiko hayo tukamueleza mlalamikaji akawaombe wamfanyie upasuaji kwa kuwa ana bima ya afya lakini watuhumiwa hao walikataa,” amesema Makungu.
Amesema watuhumiwa hao walimuambia mzee huyo endapo hatatoa fedha hizo wataandika taarifa ili apelekwe hospitali ya rufaa ya Dodoma ambapo gharama zitaongezeka za malazi na nauli.
Amesema kwa kuzingatia Dokta Kongora alikuwa mtaalamu pekee na hali ya mgonjwa ilikuwa mbaya walielekeza rushwa hiyo wapewe wataalamu hao wa afya wakati ushahidi wa kuomba na kupokea rushwa ukiendelea kukusanywa.
“Tuliacha wamfanyie upasuaji mgonjwa ambapo walifanya upasuaji huo kwa ufanisi na vile vile tulisubiri pia mgonjwa apone na kuruhusiwa kutoka hospitali ndipo tulimkamata,” amesema Makungu.
Amesema Takukuru mkoani Manyara inakemea kwa nguvu zote watumishi wachache wa Wizara ya Afya wanaokiuka maadili ya taaluma yao na kujihusisha na vitendo vya rushwa na wataendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi wa aina hiyo.
“Ni rai yetu kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa bila woga kwa kuwa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 ina vifungu vinavyowalinda wanaotoa taarifa kwa nia njema,” amesema Makungu.