Meneja wa shule ya sekondari Mguta iliyopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Monica Mlemeta akizungumza shuleni hapo.
Mandhari ya shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Wilayan Simanjiro Mkoani Manyara, yenye kutoa elimu bora na mazingira mazuri ambayo imeanzisha kidato cha tano na cha sita.
************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHULE ya Sekondari Mgutwa ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imekuwa shule ya tatu Wilayani humo kuanzisha masomo ya elimu ya sekondari ya kidato cha tano na cha sita.
Hata hivyo, Mgutwa inakuwa shule ya kwanza isiyo ya Serikali kuanzisha sekondari ya kidato cha tano na cha sita kwenye Wilaya ya Simanjiro yenye shule tatu za kidato cha tano na cha sita, nyingine ni shule ya sekondari Simanjiro na shule ya sekondari, Emboreet ambazo ni shule za Serikali.
Mkurugenzi wa shule ya sekondari Mgutwa, Shedrack Mlemeta, alisema hivi sasa wanapokea wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Tanzania, ambao wamefaulu kwenda kidato cha tano ili wasome kwenye shule hiyo yenye kutoa elimu bora na yenye mazingira mazuri.
Mlemeta anasema hivi sasa shule hiyo pia ina wafundisha wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita, hivyo wadau wa elimu wachangamkie fursa hiyo ya elimu, kwa ajili ya kuwapatia watoto wao.
Anasema baada ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2006 kuwa na maendeleo mazuri kwenye taaluma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, hivi sasa wanaendeleza hayo kwa kuanzisha kidato cha tano na cha sita.
“Tunatoa elimu bora kwa kutumia walimu bora, madarasa yenye kiwango, maabara, mazingira mazuri ya shule ambayo ipo nje kidogo ya mji mdogo wa Mirerani, tuna maji, umeme, barabara ya lami ipo na tunatoa taaluma nzuri,” anasema Mlemeta.
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Japhary Matimbwa anasema wazazi na walezi wenye watoto wanapaswa kuwarithisha elimu bora kupitia shule ya sekondari ya Mgutwa.
Anasema hivi sasa urithi wa mtoto ni elimu na siyo mashamba, mifugo au majumba, kama miaka iliyopita, hivyo wazazi watumie fursa ya uwepo wa shule ya sekondari Mgutwa kwa kusomesha watoto wao ili wapate elimu bora.
“Hapa Mgutwa mwanafunzi akipitia hapo miaka ijayo anakuwa mtu muhimu kwenye jamii kutokana na elimu bora yenye maadili mazuri inayotolewa na siyo kupata bora elimu ambayo haitamsaidia mtoto baadaye,” anasema Matimbwa.
Mkurugenzi wa taasisi ya Agape Mission International inayomiliki shule ya sekondari Mgutwa, Mchungaji Kedmon Mlemeta anasema wanajihusisha na utoaji wa elimu, maendeleo ya jamii, utume na uinjilisti.
Mchungaji Mlemeta anasema tangu mwaka 2001 waliweka mkazo katika kusaidia maendeleo ya jamii ya Simanjiro, ikiwemo kuchimba visima vya maji, maendeleo ya elimu, kilimo na upandaji wa miche ya miti ili kutunza mazingira.