………………………………………………………………….
Na Lorietha Laurence-WHUSM, Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka watumishi wapya kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumisgi wa umma wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuleta matokeo chanya kwa Serikali.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo jana Jijini Dodoma alipokuwa akifunga Mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa kwa watumishi hao wa kada ya Habari ikiwa ni tararibu ambazo hufanya kwa kila mwajiriwa mpya wa serikali.
“Natoa rai kwenu hakikisheni mnayaishi na kuyatenda yale yote mliyofundishwa na Wataalamu ili muweze kutekeleza majukumu na kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali” Dkt.Abbasi.
Aliongeza kwa kueleza kuwa Wizara hiyo inasimamia sekta za burudani ambazo huwaleta wananchi kwa pamoja na umoja bila kujali kabila wala dini ambapo ni soft power muhimu ya nchi hivyo watumishi hao walisisitizwa kuzingatia utaalamu, weledi na ufanisi wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kuleta manufaa kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
Aidha Dkt. Abbasi aliwataka watumishi hao kuwa mabalozi wazuri katika kutunza siri za serikali , kufanya kazi kwa ushirikiano, kuwa na mahusiano mazuri na watumishi wengine, kuweka malengo katika utendaji wao wa kazi ndani na nje ya utumishi wa umma ili kuwezesha kufikia malengo yaliyowekwa na Wizara.
Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa kiapo cha uadilifu kwa watumishi wa umma ambacho waliapa mbele ya mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi.
Mwisho.