……………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litachochea kasi ya ukuaji wa viwanda mkoani Simiyu kwa kujenga kituo kipya cha kupoza na kusambaza Umeme wa takriban megawati 90 katika eneo la Imalilo, Bariadi Mkoani Simiyu. Mkoa huo kwa sasa una takribani Megawati 10.
Dkt. Kyaruzi ameeleza kuwa, ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Imalilo Bariadi chenye uwezo wa kusambaza takriban Megawati 100, kitajengwa sambamba na njia ya kusafirisha umeme toka Shinyanga yenye urefu wa kilomita 109.
“Ujenzi wa kituo utapunguza urefu wa njia zinazoleta umeme mkoani Simiyu kwa sasa, hivyo kuondoa changamoto ya kukatika umeme pamoja na kufikisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya uwekezaji wa viwanda” Amesema Dkt. Kyaruzi.
Dkt. Kyaruzi ameongeza kuwa, Kuelekea maandalizi ya Ujenzi wa kituo hicho mkoani Simiyu, tayari TANESCO imeshatenga eneo lenye takriban hekari 15 pamoja na maandalizi mengine kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ili kuongeza kasi ya uwekezaji mkoani humo.
Dkt. kyaruzi pia amesema kuwa upatikanaji wa umeme mwingi na wa uhakika mkoani simiyu utasaidia kukwamua Mkoa huo kiuchumi Kutokana na fursa lukuki za kiuwekezaji na uzalishaji mali zinazopatikana mkoani humo.
Bodi ya Wakurugenzi TANESCO ikiwa mkoani Simiyu ilipata pia fursa ya kukutana na viongozi wa mkoa huo pamoja na wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Simiyu kuijionea na kusikiliza mambo mbalimbali kwa lengo la kuboresha na kuimarisha huduma za TANESCO katika Mkoa huo.
Kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Festo Kiswaga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi alieleza kuwa, Wananchi wa Simiyu, wanataka kufanya miradi mingi kama viwanda vya maji, nguo, na mashamba ya umwagiliaji hivyo umeme ndio nguzo muhimu ya uwekezaji huo.
“Hivyo tunaomba miradi ya Umeme inapokuja kupitia Mkoa wa Simiyu, basi tupewe kipaumbele kwani itaongeza tija na idadi ya watu ambao watakuwa walipaji wa umeme na hivyo kuongeza mapato ya TANESCO” ameeleza Mhe. Kiswaga.