……………………………………………………………………..
Na. Aaron Mrikaria-Dodoma
Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma ambao utatoa maelekezo ya namna ya kujumuisha masuala ya kijinsia mahala pa kazi na kujenga mazingira bora na wezeshi kwa makundi mbalimbali kwenye taasisi za umma, ili mwongozo huo uwe ni chachu ya kuongeza tija kiutendaji kwa Watumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichohudhuriwa na Wakurugenzi wa Wizara zote kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha rasimu hiyo, kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA.
Dkt. Michael amewasititiza waajiri kuwa, pendekezo la urithishanaji madaraka kuzingatia suala la kijinsia lipewe umuhimu mkubwa katika utekelezaji wake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata fursa kujumuishwa kwenye mipango ya mafunzo ili kujengewa uwezo kiutendaji.
Licha ya kuafiki pendekezo la kutilia mkazo haja ya wanawake kupewa kipaumbele katika nafasi za uongozi na kuwekewa mazingira wezeshi katika utekelezaji wa majukumu yao mahala pa kazi, Dkt. Michael pia amehimiza umuhimu wa rasimu hiyo kuyawezesha makundi yote kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Dkt. Michael awetaka viongozi katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanabaini watumishi wenye vipaji maalum kutoka makundi anuai na kuviendeleza vipaji hivyo, pamoja na kuangalia namna ya kuanzisha vituo vya malezi kwa watoto katika majengo ya Ofisi za Umma ili mtumishi anayenyonyesha aweze kutumia muda wake kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kikazi.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amesema tofauti na Mwongozo wa mwaka 2010, rasimu hii inayoboreshwa imezingatia masuala ya jinsia na usimamizi wa rasilimaliwatu, hivyo muongozo huu ukiidhinishwa rasmi kutumika utakuwa ni mahususi kuratibu ujumuishwaji wa masuala ya jinsia katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwenye Utumishi wa Umma.