Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera Charles akitoa taarifa kwa Umma kuhusu zoezi la kupitia na kufanya uamuzi wa rufaa za Wagombea Ubunge leo Septemba 8, 2020 Jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………..
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la kupitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa za wagombea Ubunge zilizowasilishwa na wagombea kupitia kwa Wasimamizi mbalimbali wa Uchaguzi nchi nzima.
Kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinatoa fursa kwa wagombea wa Ubunge kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika na uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi kutokana na
pingamizi zilizowasilishwa.
Zoezi la kuzijadili na kuzitolea uamuzi rufaa hizo linaendelea na kuanzia leo, Tume itakuwa inatoa uamuzi na kuwajulisha wahusika kwa kadri rufaa hizo zitakavyokuwa zinamalizika kushughulikiwa. Leo Tume imetoa uamuzi wa rufaa 55 za wagombea Ubunge kama ifuatavyo:
- i.
Imekubali rufaa 15 na kuwarejesha wagombea katika orodha ya
wagombea.
- ii.
Imekataa rufaa 15 za wagombea ambao hawakuteuliwa.
iii.
Imekataa rufaa 25 za kupinga walioteuliwa.
Tume imechambua vielelezo, nyaraka na maelezo ya warufani na warufaniwa vilivyowasilishwa ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa Mujibu wa Sheria na kanuni za Uchaguzi. Uamuzi uliofanywa na Tume katika rufaa hizo umewarejesha baadhi ya warufani kwenye orodha ya wagombea. Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kuanzia leo, kesho na kuendelea. Wahusika wa rufaa hizo wameanza kujulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume kuanzia leo.