Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof.Charles Kihampa akifuatilia maelekezo kutoka kwa mtaalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kutembelea banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Vyuo Vikuu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Saam
Baadhi ya Wanafunzi wakifuatilia maelekezo kutoka kwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kutembelea banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Vyuo Vikuu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Saam ili kuweza kujisajili na kujiunga na Vyuo Mbalimbali.
*********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Zaidi ya Vijana elfu 40 wamejitokeza katika viwanja vya Mnazi Mmoja kufanya usajili kujiunga na elimu ya Vyuo Vikuu kutokana na Taasisi mbalimbali za Vyuo hivyo kujitokeza kwa wingi katika Maonesho ya Vyuo Vikuu kwenye Viwanja hivyo Jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yanatarajia kufikia tamati Septemba 5 mwaka huu.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof.Charles Kihampa amesema maonesho hayo ni fursa kwa wadau mbalimbali wa elimu ya Juu kwa maana wenye viwanda na wawekezaji mbalimbali ambapo wanaweza kufika na kuona huduma zinazotolewa na taasisi hizo.
“Hii imekuwa fursa kubwa kwa wale ambao wangependa kujiunga na Vyuo Vikuu wanaweza kuzipata huduma hizo moja kwa moja iwe kwa shahada ya kwanza ama Shahada ya pili na ya tatu”. Amesema Prof.Kihampa.
Aidha Prof.Kihampa amewataka vijana wanaohitaji kujiunga na elimu ya Vyuo Vikuu kuendelea kujitokeza kwa wingi kuondoa usumbufu usio wa lazima.