MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdalla Juma ‘Mshua’,amewataka Wanawake katika Nchini kuamini,kulinda na kuipigania CCM na kuhakikisha inashinda kwa kishindo mwaka 2020 kuliko Chaguzi zote zilizopita toka kuanzishwa Mfumo wa Vyama Vingi Mwaka 1992.
Amesema Serikali za Awamu ya Saba ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini wa Marais wake ambao ni Dk.Shein na Dkt.John Pombe Magufuli, wamesimamia utekelezaji wa mambo mengi ya kimaendeleo yanayokidhi mahitaji ya Wanawake na jamii nzima kwa ujumla.
Hayo ameyasema wakati akifungua Kikao cha Baraza la UWT Wilaya ya Amani kilichofanyika katika Ofisi za Wilaya hiyo Sebleni Amani Unguja.
Mhe.Asha alieleza kwamba kupitia Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 Serikali imeimarisha Huduma za Afya,Miundombinu ya Barabara,Umeme,Elimu,Mikopo kwa Wanawake yenye masharti nafuu pamoja na kutoa fursa za Uongozi kwa Wanawake katika Chama na Serikali zote mbili.
Alisema kutokana na mambo mengi ya kimaendeleo yaliyotekelezwa Nchini, Wanawake wanatakiwa kuunganisha nguvu zao bila ya kujali bila ya kujali tofauti za Vyeo,rangi na kabila wahakikishe CCM inashinda kwa ngazi zote katika Uchaguzi Mkuu ujao kwani hiyo ndio njia pekee ya kuthamini kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali.
Kupitia Mkutano huo aliwasihi Wajumbe wa Mkutano huo na Wanawake mbali mbali kuendeleza Umoja na Mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa ndani na nje ya UWT, kwa lengo la kuandaa mazingira rafiki ya kisiasa yatakayoimarisha CCM.
Aliwakumbusha Akina Mama hao kwamba pamoja na majukumu waliyokuwa nayo wanatakiwa kusimamia Malezi ya Watoto katika Maadili mema na kuhakikisha wanalindwa dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji.
Akizungumzia suala la uimarishaji wa Chama na Jumuiya hiyo, Mhe.Asha alisisitiza umuhimu wa kuongeza Wanachama Wapya wenye Sifa kisheria za kuipigia kura CCM kwa kila Uchaguzi wa Dola.
“Kila Mwanachama kwa nafasi yake aanze kuwatafuta Wapiga kura Wapya wa makundi yote wenye Sifa za kupiga kura, waelezeni mazuri mengi yanayopatikana ndani ya CCM japokuwa mengi wanayaona na kuyatambua lakini bado tuna jukumu la kuwakaribisha kwa ukarimu kwani CCM ni Chama cha Wote,,,Nyumbani kumenoga.”,alisema Mhe.Asha.
Kupitia Kikao hicho Mhe.Asha,alikabidhi Komputa Moja na Printer Moja ya Kisasa ya rangi kwa Uongozi wa UWT Wilaya hiyo ili watekeleze kwa ufanisi shughuli mbali mbali za Umoja huo.
Naye Katibu wa UWT Wilaya hiyo Ndugu Asha Mzee Omar,akisoma taarifa ya Utendaji wa kazi za UWT, alisema Viongozi,Watendaji na Wanachama wanashirikiana vizuri huku wakijipanga vizuri kukabiliana na dalili zozote za upinzani ili CCM ishinde katika uchaguzi ujao.
Amesema katika mikakati ya kuimarisha Jumuiya wamesimamia vizuri vikao vya ngazi za Matawi hadi Wilaya kuhakikisha vinafanyika kwa mujibu wa Katiba sambamba na kufanya ziara,vikao na mafunzo ya kuwajenge uwezo Akina Mama juu ya masuala mbali mbali ya kisiasa na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza Mjumbe wa Mkutano huo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Mgeni Hassan Juma, aliupongeza Uongozi wa Wilaya hiyo kwa kutekeleza masuala ya msingi ya kiutendaji yenye dhamira ya kuimasha UWT na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mjumbe wa Mkutano huo,ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Saada Ramadhan Mwendwa, alisema kupitia kikao hicho Wanawake kutoka ngazi mbali mbali za Uongozi watajengew uwezo ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Mkutano huo wa Siku Moja ulioandaliwa na UWT Wilaya ya Amani kwa kushirikiana na Wawakilishi wa Viti Maalum wa Mkoa wa Mjini Unguja.