*******************************
Ninapenda kuukumbusha umma kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, pamoja na mambo mengine, inasimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi. Miongoni mwa Sheria hizo ni Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015. Sheria hii imeweka masharti kwa raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi hapa nchini. Miongoni mwa masharti hayo ni kuwa na Kibali cha Kazi kinachotolewa na Kamishna wa Kazi.
Mnamo tarehe 28 Agosti, 2020 ilisambazwa taarifa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyotolewa na Ofisi ya Kazi Mkoa wa Dar es Salaam ikivikumbusha Vilabu vya Mpira wa Miguu kupata Vibali vya Kazi kwa ajili ya wachezaji, makocha na wafanyakazi wengine wa kigeni walioajiriwa na vilabu hivyo kabla ya kuanza kuwatumia katika shughuli za michezo hapa nchini.
Taarifa hiyo imeleta taharuki kwa wanachama na mashabiki wa baadhi ya Vilabu vya Mpira wa Miguu hapa nchini. Ninapenda kuwatoa hofu wanachama na mashabiki wa Vilabu hivyo kwamba wanaweza kuwatumia wachezaji, makocha na wafanyakazi wengine wa kigeni katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu ya Soka haijaanza, hata hivyo Vilabu vihakikishe vinakamilisha taratibu za kisheria za kuwaombea Vibali vya Kazi raia hao wa kigeni.
Ninatoa rai kwa waajiri wote nchini, wakiwemo Vilabu vya Mpira wa Miguu, kuhakikisha kwamba wanazingatia Sheria za Kazi. Ninawasihi waajiri kufanya mashauriano na Ofisi yangu endapo kunatokea changamoto yoyote katika utekelezaji wa Sheria za Kazi badala ya kukimbilia katika vyombo vya habari.