Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk Wilson Charles Mahera akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu kuteuliwa kwa wagombea pekee wa ubunge katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
……………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza majina ya wagombea 18 wa ubunge waliopita bila kupingwa katika majimbo yao wote wakitoka Chama cha Mapinduzi CCM.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk Wilson Charles Mahera wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kuteuliwa kwa wagombea pekee wa ubunge katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Dk Mahera amewataja wagombea hao kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Ruangwa) January Makamba (Bumbuli), Alexander Mnyetti (Misungwi), Sagini Jumanne Abdallah (Butihama), Vita Rashid Kawawa (Namtumbo) na Nape Nnauye wa Jimbo la Mtama.
Wengine ni Khamis Kigwangalla (Nzega Vijijini), Zedi Jumanne (Bukene), Philip Augustino (Songwe), Eng Isack Kamwelwe (Katavi), Godfrey Mizengo Pinda (Kavuu) na Tale Tale Shabani wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.
Pia yupo Kalogereris Innocent jimbo la Morogoro Kusini, Jonas Van Zeeland (Mvomero), Prof Palamagamba Kabudi (Kilosa), Ahmed Shabiby (Gairo), Job Ndugai (Kongwa) na Elias Kwandikwa (Ushetu).
Dk Mahera amesema wagombea hao wamepita bila kupingwa kufuatia wagombea wengine kwenye maeneo hayo kushindwa kukidhi vigezo vinavyowawezesha kupita na kuwa wagombea ubunge kwenye maeneo yao.