………………………………………………………………………….
NA DENIS MLOWE,IRINGA
WAANDISHI wa habari mkoa wa Iringa,wamelaani vikali na kusikitishwa kauli aliyotoa aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa juu ya wanahabari kutoripoti habari za Chadema mkoa wa Iringa.
Akizungumza na wanahabari wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika katika ofisi za klabu ya wanahabari mkoa wa Iringa (IPC) katibu wa wanahabari mkoa Iringa, Tukuswiga Mwaifumbe alisema kuwa hivi karibuni mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli ambazo zinawalaumu wanahabari na vyombo vya habari mkoa wa Iringa kwamba hawakujitokeza na kuripoti habari za Chadema.
Alisema kuwa kauli hizo ni za kusikitisha kwa mgombea huyo kutoa kauli za namna hiyo kwani matokeo yake yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa wanahabari kwani moja maneno yake yalisema kwamba ‘vyombo vya habari ambavyo haviandiki habari za chadema na mgombea wake Tundulisu vinapaswa kupuuzwa na kususiwa haingii akilini mjini mzima wa Iringa watu wamesimama halafu mwandishi anasema hakualikwa hicho ni kichocheo kinaweza sababisha unafiki na chuki miongoni mwa wananchi.
Mwaifumbe alisema kuwa wanahabari wanajiuliza habari gani za Chadema na Tundu Lissu ambazo haziandikwi vyombo vya habari anataka visusiwe na wananchi na kumkumbusha Mchungaji Msigwa kama kuna wanasiasa anayepaswa kuvishukuru vyombo vya habari kwa kumpa nafasi kwa kipindi cha miaka mitano basi ni yeye.
Alisema kuwa wanahabari wa mkoa wa Iringa wamekuwa wakilaumiwa na vyama vingine vya siasa kwa kumpa upendeleo mwanasiasa huyo lakini pamoja nafasi hizo anazopewa zawadi pekee ambayo Msigwa analipa wanahabari ni lawama na kuhamasisha wadau wavisusie vyombo vya habari hakika hii sio haki.
Aidha alisema kuwa kutokana na kauli hizo za mchungaji Msigwa wanahabri mkoa wa Iringa wametoa wito kwa wadau mkoani hapa kupuuza kauli hizo za mchungaji Msigwa kwani zimekuwa za uchochezi mbele ya jamii kwa wanahabari mkoa wa Iringa wamemtaka mchungaji Msigwa atathimini kauli anazotoa kabla ya kuzimwaga hadharani ili asiingie kwenye ule msemo wa kuchamba kwingi mwisho kujipaka kinyesi na kumtaka kuomba radhi kutoka na kauli alizotoa kwa vyombo vya habari.
Aidha Wanahabari mkoa wa Iringa wamewataka wanasiasa wengine wanaoingia katika vinyang’anyiro vya kutaka kuchaguliwa nafasi mbalimbali wasiwapangie wanahabari kazi za habari kwani wanaotambua kama ni habari ni wanahabari wenyewe kwani wanatambua wajibu na katika kufanya kazi kwa ustadi mkubwa na kanuni ambazo zimewekwa juu ya vyombo vya habar8i.
~Katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wanahabari wanatakiwa kulindwa na wadau wote kwani kazi ya wanahabari ni moja ya nguzo muhimu katika kutangaza amani, kuchochea maendeleo, kuleta umoja na amani kwenye taifa hivyo muhimu kwa wadau kuwaheshimu wanahabari pindi wanapotimiza wajibu wao.~ alisema