Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa .
…………………………………………………………………………………………..
Na. Majid Abdulkarim
Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa ametangaza kufunguliwa rasmi kwa dirisha la udahili wa shahada ya kwanza mwaka wa masomo 2020/2021.
Prof. Kihampa amebainisha kauli hiyo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.
Prof. Kihampa amesema kuwa dirisha hilo limefunguliwa leo 26 Augusti 2020 tofauti na awali ilivyokuwa imepangwa kufunguliwa August 31, 2020.
“Napenda kuwasisitiza waombaji na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Dar es Salaam kuanzia 31 Agusti 2020 ili kupata fursa ya kuonana ana kwa ana na vyuo vya Elimu ya Juu”,amesisitiza Prof. Kihampa.
Prof. Kihampa ameeleza kuwa Dirisha la udahili litakuwa wazi hadi tarehe 25 Septemba mwaka huu na kuwaasa wananchi wote kuepuka kupotoshwa na watu wanaojihita mawakala au watoa huduma ya jinsi ya kujiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu hapa Nchini.
Katika hatua nyingine Prof. Kihampa amesema kuwa Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarfa rasmi kupitia tovuti ya TCU www.tcu.go.tz tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kufanya udahili wa wanafunzi wa shahada ya kwanza pamoja na vyombo vya habari.