Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion Bw. Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya kuelekea tamasha kubwa la kuombea uchaguzi mkuu ambalo linatarajia kufanyika Agosti 23 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
*************************************
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Tamasha kubwa la kuombea uchaguzi mkuu linaloandaliwa Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotion Bw. Alex Msama limeendelea kuchukua sura mpya baada ya orodha ya waimbaji wa nyimbo za Injili kuongezeka akiwemo Mchungaji Faustin Munishi pamoja na Jacob Chengula.
Waimbaji wengine Christina Shusho, Christopher Mwangira, Bony Mwaitege pamoja na kwaya mbalimbali, huku Rose Muhando akiendelea na mazoezi ili kuhakikisha anafanya vizuri siku ya Jumapili ya Agosti 23 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion Bw. Msama, amesema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri katika nyanja zote.
“Tumejiandaa na utaratibu wote unakwenda vizuri ikwemo usalama wa kila mshiriki, kwani Jeshi la Polisi Kanda maalum wamejipanga kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa katika ulinzi” amesema Bw. Msama.
Amesema kwa tamasha hilo litaanza majira ya saa 6 mchana na kuendelea, ambapo halitakuwa na kiingilio, washiriki wote wataingia bure.
“Waimbaji wote wa injili wanaendelea na mazoezi katika kuhakikisha wanashiriki vyema kuombea uchanguzi mkuu ufanyike kwa amani na utulivu” amesema Bw. Msama.
Bw. Msama amesema kuwa maaskofu kutoka madhehebu tofauti, viongozi wa serikali na taasisi wamejipanga kushiriki siku hiyo kwa ajili kukusanyika pamoja na kuliombea taifa kufanya uchaguzi kwa amani.
“Tumepita katika mapito mbalimbali, watanzania tujitokeze tuungane pamoja katika kuliombea taifa ili uchaguzi mkuu ufanyike kwa amani” amesema Bw. Msama.