*********************************
Na WAJMW-Dodoma
Huduma za Afya kwa mama na mtoto zimeendelea kuimarika nchini baada ya uboreshwaji wa huduma za afya nchini katika kipindi cha miaka mitano toka 2015 hadi 2020.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya afya Pamoja na watumishi mbalimbali wa Wizara hiyo waliokutana jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuimarika kwa huduma hizo zimetokana na kuimarishwa miundombinu ikiwa ni pamoja na kuongezeka vituo vya kutolea huduma 1797 ambavyo Zahanati 1198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Halmashauri 99, Hospitali za Mikoa 10 ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Mara ya Mwalimu Nyerere Memorial Hospital ambayo ujenzi wake iliasisiwa na Mwalimu J.K Nyerere mwaka 1977.
“Uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwenye miundombinu ya utoaji wa huduma za afya umeongeza umeongeza vituo vya huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni kutoka vituo 192 (Vituo vya afya 115 na Hospitali za Halmashauri 77) mwaka 2015 hadi vituo 586 (Hospitali za Halmashauri 99 na vituo vya 487) mwaka 2020 ikiwa ni sawa na ongezeko la vituo 394”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Serikali imeongeza idadi ya Vituo vya huduma kwa ajili ya Watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na shida ya kupumua, uzito pungufu na maambukizo ya Bakteria (Neonatal Care Units) kutoka 14 mwaka 2015 hadi kufikia 104 mwaka 2020.
Aidha, Serikali imeongeza upatikanaji wa huduma kwa ajili ya Watoto mahututi (Paediatric ICU) katika Hospitali za Rufaa za kanda mbili mwaka 2015 hadi Hospitali za kanda sita ambazo ni Muhimbili, Bugando, KCMC, Mbeya, Benjamin Mkapa na Mloganzila.
Waziri Ummy amesema upanuzi huu umesogeza huduma muhimu kwa ajili ya dharura ya uzazi na Watoto karibu na wananchi kupitia uimarishaji wa vituo vya afya ya msingi, hivyo kuwaondolea kero na gharama kubwa walizokua wanazitumia kufuata huduma hizi mbali na maeneo yao na hivyo kuboresha Maisha.
Kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano, viashiria vikuu vya mwenendo wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vimeendelea kuimarika ikiwa ni Pamoja idadi ya wanawake wanaotumia huduma afya ya uzazi kabla ya ujauzito na baada ya kujifungua imeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2015/16 hadi asilimia 43 mwaka 2020, ongezeko la akinamama kuhudhuria kliniki imeongezeka kutoka asilimia 39 hadi asilimia 81 kufikia mwezi Juni 2020, kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 83 Juni 2020 na hivyo kuvuka lengo la Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto (2016-2020).
Waziri Ummy amesema hali hii inaashiria utafiti wa hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini utakapofanyika mwaka 2021, kiwango cha vifo vitaokanavyo na uzazi kitakuwa chini ya vifo 190 kwa vizazi hai 100,000 ukilinganisha na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 iliyotolewa mwaka 2015/16