*************************************
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mwaka 2015 hadi kufikia bilioni 270, kuboresha miundombinu ya huduma za Hospitali ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mkoa, kuongeza Madaktari katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi za chini na kuongeza vifaa tiba na vitendanishi ili kuwezesha wananchi wengi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wananchi na huduma zitolewazo na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekutana na Viongozi waandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na MSD mjini Morogoro kwa lengo la kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizi. Kutokana na kikao hicho, Serikali imefanya mambo yafuatayo;
i. Imefanya maboresho katika orodha ya Taifa ya Dawa muhimu kwa kuongeza aina ya dawa 71 ambazo hazikuwepo awali katika orodha husika na hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi. Hivyo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya tayari umeongeza dawa hizi katika kitita chake cha mafao kitolewacho kwa wanufaika wake kuanza kutumika mara moja;
ii. Kuelekeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwasilisha maboresho ya kitita cha huduma zitolewazo kwa wanachama kwa ajili ya maamuzi na kuanza kutumika;
iii. Kufanya mapitio ya utaratibu wa mikopo itolewayo kwa watoa huduma ikiwemo ya dawa, ukarabati wa vituo, vifaa tiba na vitendanishi ili kuongeza tija na kupunguza gharama;
iv. Kuainisha maeneo ya ushirikiano baina ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili Taasisi hizi zilete tija kwa wananchi kwa ujumla hasa katika maeneo ya viwanda na huduma tiba;
v. Kuelekeza Menejimenti ya MSD kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi unakuwa wa kutosha muda wote na kwa bei nafuu kwa watoa huduma kwa kuendelea kununua moja kwa moja viwandani;
vi. Kuelekeza Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kubuni na kutekeleza mikakati ya kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiunga na kunufaika na Mfuko huo ili kufikia adhma ya Serikali ya Afya Bora kwa wote.
vii. Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha inaharakisha utekelezaji wa kutambua huduma za kibingwa bobezi kama upasuaji wa moyo, tiba ya saratani na ubadilishaji viungo karibu na wananchi kwa kuanzia na Hospitali za Kanda.
Aidha, Serikali imeagiza Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kuyafanyia kazi kwa haraka malalamiko ya makato kwa watoa huduma (Hospitali) kulingana na miongozo iliyopo na kwa kufuata haki. Vilevile Hospitali zote nchini zimeonywa kuacha kufanya udanganyifu katika madai ya malipo yatokanayo na huduma wanazozitoa kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Mwisho, Serikali itaendelea kuulea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili uimarike na kuendelea kupanua wigo na ubora wa huduma kwa wananchi wote.