Baadhi ya Vibarua wa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro wakiendelea na kazi katika Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani wilayani humo.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) akimtambulisha Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga kwa wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki wilayani Hai.
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Sabaya akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wilayani humo.
Sehemu ya umati wa wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mong’are, wilayani Hai, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani. Waziri aliwasha rasmi umeme katika Chuo hicho akiwa katika ziara ya kazi.
Sehemu ya umati wa wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wilayani Hai, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, alipozungumza nao kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Chuo cha Ualimu Mong’are, wilayani humo akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, muda mfupi baada ya kuwasha rasmi umeme katika Chuo cha Ualimu Mong’are, Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Sabaya.
………………………………………………………..
Veronica Simba – Kilimanjaro
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameunda Timu maalumu inayojumuisha wataalamu mbalimbali wa Serikali ili kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro.
Alitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020 muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Chuo cha Ualimu Mong’are.
Kuundwa kwa Timu hiyo itakayoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga kunatokana na kusuasua kwa Mkandarasi husika, Kampuni ya Urban & Rural Engineering Services Ltd katika kutekeleza kazi zake.
“Timu hii maalumu ya watu sita, itafanya kazi kwa muda wa siku 14 kuanzia leo ili kuhakikisha Mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati, ifikapo Septemba 15 mwaka huu,” alifafanua Waziri.
Waziri alimwagiza Mkandarasi husika kuweka Magenge matano ya kazi katika Wilaya ya Hai ili kuharakisha kazi husika. Aidha, aliwataka Wakurugenzi wa Kampuni hiyo kuungana na Wafanyakazi wao ili kuongeza nguvu na msukumo wa kazi.
Alikemea tabia ya Wakurugenzi hao kutokufika katika maeneo ya kazi na kuwaachia wafanyakazi wao pekee ambao hata hivyo Serikali imebaini hawalipwi mishahara yao kwa wakati hivyo kuchangia kuzorota kwa kazi.
Vilevile, alitoa maelekezo kwa Wakandarasi husika kutokuondoka Hai hadi watakapokamilisha kazi hiyo.
“Ninaagiza Wakandarasi hawa wakiwemo Wakurugenzi wao, wote wasiondoke hapa Hai hadi watakapokamilisha kazi. Aidha, ninaagiza wawe wanaripoti kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Hai, kila siku saa tatu asubuhi ili tujiridhishe kuwa wapo kazini. Mkuu wa Wilaya, tusaidie kusimamia hilo,” alisisitiza Waziri.
Maelekezo mengine aliyotoa Waziri ni kwa Wakandarasi kuhakikisha vibarua wote wanavaa nguo maalumu za kazi na kuwa na vifaa vyote vinavyowalinda na madhara zikiwemo kofia ngumu, buti na soksi za mikono.
Aidha, alielekeza wafanyakazi na vibarua wote walipwe ujira wao kwa wakati huku akisisitiza kuwa Mkandarasi atakayebainika kutotekeleza maagizo hayo, atachukuliwa hatua kali za kisheria na kimkataba.
Awali, akitoa salamu za kumkaribisha Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Sabaya alipongeza utendaji kazi mzuri wa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo lakini akalalamikia utendaji unaosuasua wa Mkandarasi husika.
“Mkandarasi hajafanya kazi ya kutosha. Tulipaswa kuwa tumesimika transfoma 37 katika Wilaya yetu lakini hadi sasa amesimika transfoma saba tu.”
Waziri alimtaka Mkandarasi huyo kukamilisha kazi ifikapo Septemba 15, 2020 na akaahidi yeyé mwenyewe kwenda kuwasha rasmi umeme katika vijiji vyote vilivyosalia.
Timu iliyoundwa inajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO Makao Makuu na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Makao Makuu.