Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole kulia,akitoa elimu ya kifua kikuu jana kwa wanafunzi wa hule ya sekondari Nandembo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambapo jumla ya wanafunzi 730 wa shule hiyo wamepata elimu ya kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na kujiking katika.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo wilayani Tunduru wakimsikiliza mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani) wakati akitoa elimu ya kifua kikuu kwa wanafunzi wa shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya uchunguzi wa TB kwa wanafunzi wa Bweni kama mkakati wa kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza mtaalam wa maabara kutoka zahanati ya Nandembo kabla ya kuanza kwa zoezi la uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu lillloongozwa na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma.
……………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na Ukoma kimetoa elimu ya Ugonjwa wa kifua Kikuu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo, ikiwa ni kampeni ya Serikali kufanya uchunguzi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo lengo likiwa kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,serikali kupitia Hospitali ya wilaya imepokea mpango wa kutokomeza ugonjwa wa TB na tayari wameshaanza kuufanyia kazi kwa kufanya kampeni ya uchunguzi kwa wananchi ikiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Alisema mwezi Mach mwaka huu,Hospitali ya wilaya ilizindua rasmi kampeni ya uchunguzi katika kijiji cha Naikula iliyofahamika kwa jina la Nyumba kwa nyumba,shule kwa shule na kilinge kwa kilinge ambapo takribani watu 540 walifanyia uchunguzi na wale waliobainika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo walianzishiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Kihongole,kifua kikuu ni ugonjwa unaenezwa kwa njia ya hewa na unaosababishwa na bakteria wanaopatikana kwenye vitu mbalimbali ikiwemo maziwa ya ng’ombe yasiochemshwa vizuri.
Dkt Kihongole ambaye pia ni mratibu wa tiba asili na tiba mbadala wa wilaya hiyo alisema, kuna aina mbili za tb ambayo ni ya mapafu na nje ya mapafu ambapo tb ya mapafu ndiyo mbaya zaidi kwani inaambukiza kwa haraka na kuuwa kwa haraka na asilimia 80 ya wagonjwa wanaugua tb ya mapafu ikilinganisha na tb nje ya mapafu.
Alisema, lengo la Serikali ya Tanzania na Shirika la Afya Dunia(WHO)ni kuhakikisha inatokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035 na kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Dunia asilimia 95 ya wagonjwa wa kifua kikuu wapo Bara la Afrika na hali hiyo inatokana na umaskini.
Ametoa rai kwa jamii pindi mtu anapobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo, ni vema kwenda katika vituo vya kutolea huduma kupata tiba ambayo inatolewa bure badala ya kutumia dawa za asili ambazo hadi sasa hazijathibika kama zinatibu maradhi ya kifua kikuu.
Amezitaja dalili za kifua kikuu ni kukohoa kuanzia wiki mbili hadi tatu,kupungua uzito,kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku,kupoteza hamu ya kula na kupumua kwa shida kwa sababu bakteria wa ushambulia mapafu.
Aidha alitaja dalili kwa watoto wadogo ni kuchelewa kukua,kulia lia,kupata na utapia mlo na kupungua uzito na kuwashauri wazazi na walezi kuhakikisha kama mtoto anadalili hizo ni vizuri kumpeleka katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi.
Kihongole alitaja makundi yaliyopo katika hatari ya kupata maradhi hayo ni watu wenye umri mkubwa kwani kwa kawaida mtu mwenye umri mkubwa kinga ya mwili upungua,watu wanaokunywa pombe kupindukia,wanaoishi kwenye mikusanyiko kama shuleni,vyuoni,magereza n ahata wasafiri.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo Maria Mtenjele alisema, elimu waliyoipata imewasaidia sana kutambua dalili na namna ya kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu.
Ameiomba Serikali kupitia wizara ya Afya, kuendelea kutoa elimu ya kifua kikuu na maradhi mengine mara kwa mara ili wanafunzi na jamii wapate uelewa mkubwa kama njia ya kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwemo kuenea kwa magonjwa hayo na vifo.
Kwa upande wake Mwalimu Elias Komba amesema, elimu iliyotolewa na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu imesaidia sana wanafunzi kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu,dalili na jinsi ya kuchukua tahadhari kwani pia wanafunzi watakuwa mabalozi wazuri kwa wazazi na jamii pindi watakaporudi nyumbani.