***********************************
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, inamshikilia Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimana Wilson Ngolanya (63) kwa tuhuma za rushwa ya ngono.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Babati na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, Mwenyekiti huyo Ngolanya alikamatwa Agosti 15 mwaka huu kwenye nyumba ya kulala wageni ya Naisimo iliyopo mjini Kibaya.
Makungu amesema Mwenyekiti huyo wa kijiji alikutwa uchi wa mnyama akiwa amevalia kondomu tayari kwa kutekeleza uhalifu huo.
Amesema awali walipokea taarifa toka kwa mlalamikaji binti wa miaka 23 (jina lihahifadhiwa) akimtuhumu Mwenyekiti huyo wa kijiji kwa kumuomba rushwa ya ngono.
“Kwa mujibu wa uchunguzi Ngolanya alikuwa akiomba rushwa ya ngono ili aweze kumsaidia mlalamikaji kuwaondoa wavamizi watatu shambani,” amesema Makungu.
Amesema shamba hilo lilikuwa linamilikiwa na baba wa binti huyo ambaye kwa hivi sasa ni marehemu.
“Uchunguzi unaonyesha kuwa Ngolanya anafahamu kuwa shamba hilo lilikuwa la marehemu baba wa binti huyo, hata hivyo alimtaka binti huyo ampe rushwa ya ngono ili aweze kuwaondoa wavamizi hao,” amesema.
Amesema binti huyo baada ya kuona usumbufu unazidi alitoa taarifa TAKUKURU na baada ya kujiridhisha na uchunguzi wa awali makachero waliweka mtego.
Amesema mtego huo ulifanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo ya kulala wageni iitwayo Naisimo akiwa tayari amevua nguo zake zote na kuvaa kondomu ili kutimiza uhalifu huo.
“Kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 kinasema mtu aliye kwenye mamlaka au uongozi ambaye kwa kutumia mamlaka au cheo alichonacho akilazimisha rushwa ya ngono ili aweze kumpa mtu yeyote ajira, kupandishwa cheo, kumpa haki stahiki, upendeleo au unafuu usiostahili anakuwa ametenda kosa la rushwa ya ngono,” amesema Makungu.
Amesema ikithibitika kuwa amehusika na kitendo hicho adhabu ya faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja.
“Rai yetu kwa viongozi wachache ndani ya utumishi wa umma na binafsi wenye tabia na fikra kama za Ngolanya za kuomba rushwa ya ngono waache mara moja kwa kuwa sheria ni msumeno unakata mbele na nyuma,” amesema Makungu.
Amewaomba pia mabinti pale wanapokutana na kudaiwa rushwa ya ngono kinyume na kifungu cha 25 PCCA namba 11/2007 kama ilivyofafanuliwa hapo juu watoe taarifa TAKUKURU kwa namba ya dharura 113 au ofisi za TAKUKURU mkoa na wilaya zilizopo karibu ili kuwaondoa hawa wachache wanaotumia vyeo walivyonavyo kudhalilisha utu kwa kulazimisha rushwa ya ngono.