UONGOZI wa Wilaya ya Kibiti umetekeleza maagizo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga choo katika stendi ndani ya siku saba. Pichani, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mwananchi baada ya kukagua na kuridhishwa na utekelezaji wa agizo hilo, Agosti 13, 2020. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gulamhussein Shaban na kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya ya Kibiti, Mohammed Mvula. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********************************
*Ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Magufuli
UONGOZI wa Wilaya ya Kibiti umetekeleza maagizo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga choo katika stendi ndani ya siku saba.
Hayo yamebainika leo (Alhamisi, Agosti 13, 2020), mara baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kukagua ujenzi wa choo hicho kama iliyoagizwa.
Akizungumza na wakazi wa Kibiti waliojitokeza katika stendi hiyo, Waziri Mkuu amesema viongozi wanapaswa kupanga ratiba za kuwasikiliza wananchi na siyo kuwaacha wasubiri viongozi wakuu ndipo watoe kero zao.
“Hivi ni kazi ya Rais wa nchi kuagiza kwamba choo kijengwe? Mlikuwa wapi siku zote kukijenga, na sasa mbona mmemaliza kukijenga ndani ya siku saba? Hizo fedha mmezipata wapi?”
“Kama mmeweza kujenga choo cha kisasa ndani ya siku saba, ina maana ndani ya mwezi mmoja mngejenga vyoo vingapi? Ni kwa nini mnasubiri maelekezo ya Mheshimiwa Rais ndipo mjenge, kwani hamkujua kwamba hapa ni mjini na panastahili kuwa na choo?” alihoji Waziri Mkuu.
Alisema viongozi wanapoteuliwa kuongoza wananchi, wanakuwa wameaminiwa na Mheshimiwa Rais; na jukumu lao kubwa la kwanza ni kwenda kuwatumikia wananchi. “Kazi yenu ya kwanza ni kutatua kero za wananchi, siyo kuwaacha wasubiri hadi anapopita Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Lazima mpange ratiba za kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ambaye alitoa nafasi kwa wananchi watatu waulize maswali, alisema maswali yao yote ni makini lakini yameulizwa kwake kwa sababu hakuna kiongozi aliyeenda kuwasikiliza.
Maswali hayo yalihusu marejesho ya mikopo kutoka benki ya Equity ambapo wakulima walikopeshwa fedha lakini wameshindwa kurejesha sababu ya mvua nyingi zilizonyesha na kuharibu mazao yao.
Alimwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Gulamhussein Shaban Kiffu ahakikishe anawasikiliza wananchi hao na wao wampe ahadi yao ya marejesho (commitment) kisha awasiliane na benki hiyo.
Kuhusu upatikanaji wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya vitatu vilivyopo Kibiti na hospitali ya wilaya, Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa wilaya afuatilie upatikanaji wa dawa kwenye vituo hivyo ili wananchi wasiendelee kupata shida.
Alisema tangu Rais Magufuli aingie madarakani, amekuwa akipigania kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa dawa hospitalini. “Serikali ya awamu ya tano imeongeza bajeti ya dawa na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 30 hadi shilingi bilioni 269 kwa mwaka, na kwa hiyo wananchi hawapaswi kukosa dawa kwani hivi sasa upatikanaji wa dawa katika maeneo mengi nchini umevuka asilimia 90.”
Kuhusu ubovu wa barabara ya katika kijiji cha Kikale, wilayani humo, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya afuatilie suala hilo.
Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe maelezo kuhusu barabara iliyoulizwa na Bw. Hemedi Hamisi, mkazi wa kijiji cha Kikale, Mhandisi wa TARURA wilayani humo, Mhandisi Salim Bwaya alisema barabara hiyo iko kwenye tangazo la zabuni mkoani.
Alisema barabara husika ni ya Muyuyu – Ruaruka yenye urefu wa km.25 na kwamba kijiji cha Kikale, kimo miongoni mwa maeneo korofi ya barabara hiyo.