Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad akizungumza na Washiriki wa Mkutano wa Tathmin ya Dawa huko Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar (Kulia) Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Halima Salum na Mratibu wa Huduma za Ushaurinasaha na Uchunguzi wa Virusi vya Ukumwi Tatu Bilali
Afisa kutoka Ofisi ya Mfamasia Mkuu wa Serikali Said Mohamed akieleza mpango mkakati wa dawa katika mkutano wa tathmini uliyofanyika Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi nje kidogo ya Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad akiwatembeza washiriki wa mkutano wa tathmini ya dawa baada ya kumaliza mkutano wao wa siku moja maelezo. (Kushoto) ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Halima Salum.
Meneja Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Lydia Zungufya akiongoza washiriki wa mkutano wa tathmini ya kuangalia uhifadhi wa dawa kabla ya kupelekwa hospitali na vituo vya afya.
*****************
Na Ramadhani Ali – Maelezo 27.6.2019
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya Halima Maulid Salum ameshauri kuongeza ushirikiano baina ya watendaji wa Taasisi zilizomo ndani ya Wizara hiyo na Halmashauri za Wilaya katika kufanikisha usambazaji wa dawa kwenye vituo vya afya baada ya Serikali kufanya ugatuzi katika huduma za afya ya msingi.
Amesema suala la ugatuzi ni kitu kipya kwa Zanzibar, na watendaji wengi bado hawajauelewa vizuri, hivyo suala la ushirikiano na ufuatiliaji wa mara kwa mara ni jambo la msingi katika kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Naibu Katibu Mkuu alitoa ushauri huo Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi katika mkutano wa kutathmini utaratibu mzima wa uagiziaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa katika hospitali na vituo afya.
Alisema kumejitokeza malalamiko kwa baadhi ya Halmashauri za Wilaya, hawatoi ushirikiano mzuri kwa Wafamasia wa Wilaya zao na hatimae baadhi ya vituo hukosa dawa na vyengine kuwa na mrundikano mkubwa wa dawa bila kuwa na matumizi na hatimae kumaliza muda wa matumizi.
Alisema upatikanaji wa dawa Zanzibar hivi sasa upo vizuri kufuatia Wizara ya Afya kuongezewa bajeti ya kununulia dawa na jambo la msingi ni kuhakikisha zinatunzwa vizuri zinapofika kwenye vituo vya afya.
Mkurugenzi wa Bohari kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad amewahakikishia wadau wa Dawa walioshiriki mkutano huo kwamba wataendelea kutoa huduma bora kwa wakati kwenye hospitali na vituo vyote vya afya Unguja na Pemba.
Hata hivyo aliwataka wananchi wanapopata tatizo la afya kufika hospitali na vituo vya afya na kuhakikisha dawa wanazopewa wanazitumia kwa usahihi.
Alisema baadhi ya wananchi huchukuwa dawa na kuzitumia kwa muda mfupi na baada ya kupata nafuu huzitupa bila ya kujua kwamba Serikali imetumia fedha nyingi kuziagiza.
Aidha aliwataka wafanyakazi wa Bohari Kuu kuendelea kutimiza wajibu wao wa kuhudumia jamii ya Zanzibar kwa uadilifu na mapenzi makubwa.
Mkutano huo wa siku moja wa wadau wa dawa uliangalia mafanikio yaliyofikiwa katika mfumo mzima wa dawa, changamoto na njia za kupunguza changamoto zilizojitokeza na njia za kuzitafutia ufumbuzi changamto hizo.