Dkt. Omar Kasuwi (wa pili kushoto) akiteta jambo na Viongozi kutoka Kiwanda cha Alliance One Tobacco kabla ya makabidhiano ya Mashine hizo za kusaidia kupumua,kushoto kwake ni Daktari wa Kampuni Dkt. Mosi Makau, Bwana Blasius Lupenza ambaye ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Kiwanda hicho na wa kwanza kulia ni Dkt. Elimwidimi Swai Dakatari kiongozi wa Hospitali ya SUA upande wa Mazimbu.
Daktari Mkazi wa Hospitali za SUA, Dkt. Omar Kasuwi wa pili kulia akipokea Moja ya Mashine hizo nne za kusaidia kupumua kutoka kwa Mkurugenzi wa rasilimali watu wa Kiwanda cha Alliance One Tobacco bwana Blasius Lupenza.
Katibu wa Hospital za SUA bwana Banzi akikagua Mashine hizo nne kutoka kwenye mabox kabla ya makabidhiano rasmi kati ya SUA na Kampuni ya Alliance One Tobacco, wa pili kutoka kushoto ni Dkt. Omar Kasuwi, Dkt. Mosi Makau kutoka Alliance zone Tobacco, Bwana Blasius Lupenza Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Kampuni na Wa kwanza kulia ni Dkt. Elimwidimi Swai Daktari kiongozi wa Hospitali ya SUA upande wa Mazimbu.
******************************
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika kupambana na Ugonjwa wa COVID 19, Uongozi wa kiwanda cha Alliance One Tobacco kimetoa mashine mpya nne za Oxygen kwa hospitali ya SUA ili kuiongezea uwezo zaidi wa kutoa huduma kwa wagonjwa wake.
Akikabidhi mashine hizo za kusaidia kupumulia Mkurugenzi wa rasilimali watu wa Kiwanda cha Alliance one tobacco Bwana Blasius Lupenza amesema lengo la kutoa mashine hizo nne ni katika kuongeza jitihada za kupambana na ugonjwa wa Covid 19 na kwamba ijapokuwa tayari Mungu amelisaidia taifa letu katika kuondoa ugonjwa huo lakini ni lazima jitihada za kibinadamu ziendelee.
‘’Hizi mashine za kusaidia kupumua zitasaidia jamii inayotuzunguka hapa morogoro na watu wengine mbalimbali wanaofika kwenye hospitali hii wakiwa na hiyo shida ili afya za watanzania ziendelee kuwa salama maana vifaa hivi ni vinahitajika sana kwenye kuokoa maisha ya watu wenye maambukizi ya virusi vya Corona ambao wapo katika hali mbaya kwa kushindwa kupumua’’ Alifafanua Bwana Lupenza.
Akizungumzia sababu ya wao kuchagua kupeleka mashine hizo kwenye hospitali ya SUA bwana Lupenza amesema Hospitali ya SUA katika kipindi chote cha mlipuko wa ugonjwa huo imefanya kazi kubwa sana katika kusaidia kutibu na kuokoa maisha ya wagonjwa COVID 19, lakini pia miundombinu mizuri japo ina vifaa hivyo vichache vya ina hiyo lakini kuwapa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza jitihada zao za kuokoa maisha ya Watanzania wengi zaidi.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Daktari kiongozi wa Hospitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi ameushukuru uongozi wa Kiwanda cha Alliance One Tobacco kwa kuona umuhimu wa kutoa mashine hizo kwenye hospitali hiyo na kusema kuwa vifaa hivyo ni moja kati ya mahitaji ya muhimu kwenye jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID 19.
Dkt. Kasuwi amesema pamoja na kwamba kuna utulivu kidogo kwenye uhonjwa huo hapa nchini kama ambavyo viongozi wakuu wa Serikali wanavyoeleza lakini wamekuwa wakisisitiza jamii kuchukua tahadhari zote kwani sio kwamba ugonjwa umeisha kabisa hivyo kupata vifaa hivi ni moja ya muendelezo wa kuchukua tahadhari zinazoolewa na Serikali.
‘’Mpango huu wa kupata vifaa hivi leo umeanza miezi mitatu iliyopita ambapo umepitia katika hatua mbalimbali za mazungumzo na tathimini ya mahitaji lakini tunashukuru kuona leo tunakabidhiwa vifaa hivi muhimu kwenye hospitali yetu na kutuongezea uwezo zaidi wa kutoa huduma kwa wahitaji’’ Alisema Dkt. Kasuwi.
Tangu kulipuka kwa ugonjwa huo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimefanya jitihada kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambapo hospitali za SUA zimeshiriki kikamilifu kusaidia kutibu na kuokoa maisha ya wagonjwa hao lakini pia maabara ya SUA iliyopo kwenye ndaki ya tiba za wanyama za sayansi za afya iliteuliwa kuwa moja maabara zilizotumika katika kufanya uchunguzi wa sampuli za washukiwa wa Ugongwa wa Covid 19 nchini.
Wakati wa ufungaji wa maonesho ya kilimo nanenane kanda ya mashariki Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametumia nafasi hiyo kuishukuru SUA kwa msaada na mchango mkubwa walioutoa katika zoezi la upimaji wa sampuli hizo za washukiwa wa ugonjwa wa COVID 19 kwa ubora wa hali ya juu.