Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi Meneja wa Mauzo wa AFRICAB Johnson Mabesa Cheti Cha Ushindi katika Maonesho hayo.Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stellah Manyanya akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la maonesho la AFRICAB katika maonesho hayo ya Kanda ya kati.
*********************************
KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro Cables(AFRICAB) imeahidi kuendelea kuzalisha bidhaa bora ili kukidhi matakwa ya wananchi na Serikali kwa ujumla
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kampuni hiyo kuibuka na ushindi wa pili katika kundi la wazalishaji wa vifaa vya Ujenzi kikiwakilisha taasisi zinazojihusisha na sekta ya umeme katika kilele cha maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima(NANE NANE)Kanda ya Kati yaliyofanyika eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
Ushindi huo wa nafasi ya pili kwa AFRICAB ukitanguliwa na nafasi ya kwanza iliyochukuliwa na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), umetokana na jitihada za kampuni hiyo katika uzalishaji wa kiwango bora kwa vifaa mbalimbali vya umeme zikiwemo nyaya, Pipeline(PVC), Transfoma, soketi na vinginevyo hatua iliyoifanya kampuni hiyo kuzidi kujizoelea umaharufu.
Kampuni hiyo pia inazalisha nyaya za msongo mkubwa wa umeme zinazotumia katika miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwaa na Serikali ikiwemo ya Bwawa la kuzalisha umeme la Mto Rufiji maarufu kama Bwawa la Nyerere, ujenzi wa mradi wa Treni ya Kisasa ‘Standard Gauge (SGR) pamoja na miradi ya usambazaji wa umeme Vijini (REA).
Tuzo hiyo ikihusisha cheti cha kutambua mchango wa kiwanda hicho katika ujenzi wa kiuchumi wa Taifa ambayo hivi karibuni limetangazwa kuingia uchumi wa kati, ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ambaye alikuwa mgeni Rasmi wa maonyesho hayo kwa Kanda ya Kati ambapo Kitaifa yamefanyika mkoani Simiyu.
Akizungumza wakati wa utoaji wa tuzo hizo, Dkt Nchimbi pamoja kuzipongeza taasisi zote zilizoibuka na ushindi katika maonyesho hayo, pia alimpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuiingiza Tanzania kwenye uchumi wa Kati na kuwaomba watanzania kumchagua tena katika kipindi kijacho ili maono yake ya kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kwa kasi itimie.
“Kwa mkoa wa Singida tumejipanga kuhakikisha tunaunga mkono jitihada hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika mkoa huo”alisema Dk Nchimbi
Aidha akizungumza baada ya kupokea tuzo kwa niaba ya Kampuni hiyo ya Kilimanjaro(AFRICAB) Meneja Mauzo wake Jonson Mabesa, pamoja na kuishukuru Kamati ya maandalizi kwa kutambua juhudi zinazofanywa na AFRICAB katika kuliletea Taifa maendeleo, alisema malengo ya kampuni hiyo ni kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kutumiza malengo iliyojiwekea.
Alisema wao kama wazalishaji wa vifaa bora na vya kisasa vya umeme nchini na Afrika Mashariki na Kati, wataendelea kuhakikisha wanazalisha vifaa vyenye ubora ili kuendana na mahitaji ya soko sambamba na kuondoa dhana ya hapo zamani kuwa ni lazima kununua vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi.
“Kama ilivyo desturi yetu, AFRICAB tutazidi kuhakikisha bidhaa mbalimbali tunazozizalisha zinakuwa ni zenye ubora wa hali ya juu ili kukidhi matakwa ya kila mwananchi na kumuepusha kupata hasara ya mali yake hasa pale anapokwenda kununua bidhaa zisizo na ubora, kwetu ni sehemu salama na yenye kujali thamani ya fedha ya kila mwananchi” alisema Mabesa
Hivi karibuni Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo alitembelea kiwanda hicho cha AFRICAB kujionea uzalishaji unaofanyika na kuridhishwa na uzalishaji huo na kisha kuziagiza Ofisi zote zilizopo chini ya mamlaka yake kuhakikisha wananunua bidhaa za umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani hususani zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Aidha alisema kwa sasa haoni haja ya watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini kutoka nje ya nchi kutokana na uwezo wa viwanda vya ndani wa kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi matakwa ya walaji.