Baadhi ya wachezaji wanaoshiriki mchezo wa mpira wa kengele kutoka mikoa mbalimbali wakichuana katika hatua ya makundi ambapo jumla ya mikoa 23 yenye timu za wavulana na wasichana inashiriki mchezo huo unaofanyika katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara
…………………….
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Mikoa 23 kati ya 26 ya Tanzania bara inashiriki mchezo wa mpira wa kengele katika mashindano yanayoendelea katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
Ukiacha mikoa ya Katavi, Simiyu, na Songwe, mikoa mingine yote imeleta washiriki ambapo mchezo huu unaochezwa kwa dakika 24, dakika 12 kila upande na dakika 5 za mapumziko umekuwa kivutio cha aina yake hapa Mtwara.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa michezo hiyo bwana John Ndumbaro, bingwa mtetezi wa michuano hiyo kwa upande wa timu ya wasichana ni mkoa wa Tabora na kwa wavulana bingwa ni mkoa wa Morogoro.
Mchezo huu huchezwa na washiriki watatu wasioona, au wenye uono hafifu ambao hufungwa vitambaa usoni, ambapo mchezaji atalazimika kuucheza kwa kutumia hisia za kengele kwani mpira wenyewe unapoburuzika ni rahisi kuusikia mlio wa kengele hivyo na utazuiwa kwa kuudaka.
Amesema goli likiingia refa atapuliza filimbi mara mbili, na endapo mchezaji atarusha kuelekea upande wa pili ukiwa juu bila kuburuzika, refa atapuliza filimbi kutoa adhabu ya penati ambapo refa atawatoa wachezaji wawili na kumbakisha mmoja ili aweze kudaka penati.
Ndumbaro amesema goli linalotumika kwa kila upande lina upana wa mita 9 wakati uwanja mzima una ukubwa wa mita 18 sawa na uwanja unaotumika kwa ajili ya mpira wa wavu (volleyball).
Amesema kuwa mashindano ya mpira wa kengele sasa ipo katika hatua ya makundi ambapo katika michezo iliyochezwa jana Pwani wavulana ilifungwa na Kigoma kwa magoli 0-15, Dar es salaam wavulana iliifunga Mara 13-09, Arusha wasichana iliifunga Mbeya 9-7, Mara wasichana waliifunga Kigoma 10-0, Kilimanjaro wavulana waliifunga Tabora 6-3, Pwani wasichana walifungwa na Tabora magoli 3-23, Mbeya wavulana walitoka sare na Arusha kwa magoli 8-8, Dar es salaam wasichana iliifunga Iringa 19-8, Morogoro wasichana waliifunga Ruvuma 8-2.
Matokeo ya michezo mingine yanaonyesha kuwa Rukwa wavulana walitoka sare na Iringa 8-8, Tanga wavulana waliifunga Pwani 10-0, Ruvuma wavulana waliifunga Kagera 14-10, Lindi wavulana walitoka sare na Njombe 14-14, Iringa wasichana walifungwa na Morogoro 4-17, Mtwara wasichana walifungwa na Mbeya 2-17, Mara wavulana waliifunga Iringa 14-4, Tabora wavulana waliifunga Geita 14-3, Mwanza wavulana waliifunga Kigoma 13-5, Ruvuma wasichana waliifunga Rukwa 12-2.
Pia Dar es salaam wavulana waliifunga Rukwa 23-9, Shinyanga wavulana walifungwa na Geita 9-16, Pwani wavulana waliifunga Manyara 10-6, Singida wavulana waliifunga Kagera 10-8.