Na Lydia Churi-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa
Mahakama kubadili tabia na mitazamo ili iendane na ubora wa majengo mapya na
yenye vifaa vya kisasa yanayojengwa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo
mbalimbali nchini.Akizindua jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga leo, Jaji Mkuu amesema
Mahakama haitokani na majengo mazuri peke yake, bali huduma bora kwa
wananchi ambapo pia amewataka watumishi wa Mahakama kuacha tabia
zisizoendana na maadili mema wanapotekeleza wajibu wao.“Maboresho makubwa tuliyofanya kupitia Mpango Mkakati, Programu ya
Maboresho na uwekezaji mkubwa katika TEHAMA hayataboresha huduma za
utoaji haki kama watumishi na viongozi katika ngazi zote za Mahakama
hawatakuwa na mitazamo chanya ya kuwaheshimu na kuwathamini wanaofika
mahakamani kutafuta haki” alisema Jaji Mkuu.
Alisema, nguvu na uwezo wa Mahakama kwa kiasi kikubwa unategemea imani ya
wananchi kwa Mhimili huo na kuwa dhana ya sasa inayoongoza ujenzi wa
majengo ya Mahakama ni kujenga majengo yanayotoa huduma jumuishi
(Integrated Justice Centres), yaani kutoa huduma za zaidi ya ngazi moja ya
Mahakama na pia wadau wanaotoa huduma mbali mbali kuwa katika jengo moja.
Jaji Mkuu alisema maboresho yatakuwa endelevu endapo watumishi wote
watayaelewa na kutambua Mahakama inaelekea wapi. “Nawaomba watumishi wa
Mahakama tutekeleze dhana ya kumiliki maboresho na tutafanikiwa endapo kila
mtumishi atafuatilia utekelezaji wake na kuyaelewa na kuwa tayari kuyafafanua
kwa wananchi, wadau na hata kwa Mihimili ya Serikali na Bunge” alisisitiza.
Alisema maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama yanalenga mambo
makuu mawili ambayo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za utoaji haki
katika majengo bora yakiwa na vitendea kazi vya kutosha na kuwapunguzia
wananchi umbali mrefu wanapotafuta huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu aliwapongeza wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kupewa
kipaumbele katika kupatiwa huduma za Mahakama Kuu kwani mikoa ya
Morogoro, Pwani, Singida, Manyara, Njombe, Geita, Katavi, Lindi, Simiyu na
Songwe bado inasubiri kwa hamu kuwa na majengo yao ya kutoa huduma katika
ngazi ya Mahakama Kuu.
Pamoja na kusogezewa huduma katika ngazi ya Mahakama Kuu; wananchi wa
Mkoa wa Shinyanga, kupitia jengo lililozinduliwa wamesogezewa pia huduma za
Mahakama ya Rufani. Kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe
24/7/2020, jengo la Mahakama Kuu Shinyanga, limetangazwa kuwa ni Masjala
Ndogo ya Mahakama ya Rufani.
Alifafanua kuwa tangazo hilo lina maana kuwa, Mahakama ya Rufani itafanya
kikao chake cha kwanza Shinyanga kuanzia tarehe Agosti 10 hadi 28, 2020 ili
kusikiliza jumla ya mashauri 29. Kila mwaka, Mahakama ya Rufani itakuwa na
vikao katika jengo kanda ya Shinyanga.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kubuni na kuendeleza mkakati
wa ujenzi wa majengo ya Mahakama yenye ubora zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack aliipongeza Mahakama
ya Tanzania kwa kusogeza karibu na wananchi. Alisema kazi ya Mhimili wa
Mahakama pamoja na Serikali ni kutoa huduma bora kwa wananchi ili wawe na
furaha na amani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi
amesema Mahakama ya Tanzania imejipanga kama mihimili mingine ilivyojipanga
katika suala la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu.
“Mahakama itasimama kwenye nafasi yake katika uchaguzi Mkuu”alisisitiza Jaji
Kiongozi.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka
watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuyalinda, kuyaenzi na kuyaishi
maboresho ya Mahakama ikiwemo majengo pamoja na matumizi ya Tehama.
Aliwataka watumishi kutenda haki na kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na
uadilifu.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru
alipongeza watangulizi wake Mahakama kwa ubunifu na usimamizi mzuri wa
miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama likiwemo jengo la kanda ya Shinyanga
lililozinduliwa.
Akizungumzia gharama za ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Bw. Leonard Magacha amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu
zaidi ya shilingi bilioni 3.9 ambazo ni fedha za ndani.