Baadhi wa wanafunzi wa Masomo ya Umahiri Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta alipotembelea Kampasi hiyo
Mkuu wa Kampasi ya Dar es Salaam ya Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Honest Ngowi akiwa ameambatana na Mkuu wa Chuo na Menejimenti ya Chuo hicho walipowasili kukagua miundombinu ya ujenzi Tawi la Chuo Kikuu Mzumbe
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta akiwa na viongozi wa juu wa chuo hicho, akiangalia kwa makini ubora wa samani zilizofungwa kwenye moja ya madarasa yatakayotumika Tawi la Tegeta.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta (Katikati wa kwanza kushoto) akiwa amekaa kwenye Viti katika moja ya madarasa yaliyokamilika Tegeta Kampasi ya Dar es Salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka na wa mwisho kushoto ni Prof. Ganka Nyamsogoro Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma. Kulia wa kwanza ni Prof. Honest Ngowi Mkuu wa Kampasi ya Dar (mwenye shati jeupe) akifuatiwa na Prof. Ernest Kihanga Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha na Utawala.
Mkuu wa Kampasi ya Dar es Salaam ya Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Honest Ngowi (aliyevaa Barakoa) akimwonesha Mkuu wa Chuo michoro na ripoti ya maendeleo ya ukarabati na Ujenzi wa Madarasa Tegeta.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti na wafanyakazi wa Kampasi ya Dar es Salaam alipotembelea Kampasi hivyo
…………………………………………………………………………….
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta amefanya ziara ya kikazi Kampasi ya Dar es Salaam na kupongeza jitihada kubwa zilizofanyika za kupandisha hadhi Kampasi hiyo kuwa Ndaki “Campus College”.
Katika ziara hivyo Mhe. Samatta aliongozana na Makamu Mwenyekiti wa Baraza CPA. Pius Maneno, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof Lughano Kusiluka na wajumbe wa Menejimenti; na kuzungumza na Wafanyakazi, Wanafunzi na kukagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa miundombonu Tegeta, eneo ambalo limeandaliwa kwa ajili ya masomo ya Shahada za Kwanza mwaka wa masomo 2020/2021.
Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya Chuo hicho, Mhe. Samatta ameupongeza uongozi kwa jitihada na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya muda mfupi Tegeta, akilinganisha na taswira aliyoiacha wakati alipofanya ziara yake ya mwisho mwaka jana 2019.
“Nimefarijika sana kuona mabadiliko haya makubwa kwakweli sikutegemea. Ila nina imani kubwa kituo hiki kitafungua fursa nyingi na kuongeza idadi ya wananchi wanaotaka kujiendeleza na Elimu ya Juu, kwakuwa hapo awali walilazimika kwenda kufuata masomo ya shahada za awali kwenye Kampasi zetu Morogoro au Mbeya…” akisisitiza
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa Lughano Kusiluka, amesema tayari Chuo kimeshapata idhini ya kuanzisha kozi za awali Tegeta kutoka Tume ya Vyuo Vikuu(TCU) na kwamba wanaendelea na hatua za mwisho za maandalizi ya miundombinu kwaajili ya kupokea wanafunzi kwa mwaka ujao wa masomo na kwa kuanza wataanza na kozi mbili za awali ambazo ni Shahada ya Utawala wa Umma (Bachelor of Public Administration -BPA) na Shahada ya Uhasibu na Fedha- Sekta ya Biashara (Bachelor of Accountancy and Finance- Business Sector (BAF-BS).
Ziara ya Mkuu wa Chuo Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta ni sehemu ya utaratibu aliojiwekea kila mwaka wa kutembelea Kampasi zote zilizopo chini ya Chuo hicho, kukagua shughuli na miradi ya maendeleo, kuzungumza na Wafanyakazi na Wanafunzi, pamoja na kujibu hoja mbalimbali. Hii ni ziara yake ya mwisho kufuatia muda wake wa uongozi kufikia tamati ambapo tarehe 13 Januari 2021 atakuwa ametimiza miaka 11 ya uongozi wake tangu alipoteuliwa mwaka 2009 na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.