***********************************
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Tanzania imekuwa kati ya nchi za kwanza kufungua anga kwa kuruhusu safari za ndege kutoka nchi mbalimbali duniani kutua nchini baada ya usafiri wa anga kusitishwa kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19 lililoikumba dunia mwezi Desemba mwaka 2019.
Jitihada hizo za Serikali za kurejesha safari za ndege baada ya athari ya ugonjwa wa Covid-19 zimekuwa na manufaa ambapo jana (Agosti 5, 2020) ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) aina ya Boing 777-200 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikibeba watalii.
Mashirika mengine ya ndege zilizoanza safari zake nchini ni pamoja na Shirika la Ndege la Ethiopia, Dreamliner, Boing kutoka Marekani na Gulfstream la Coratia. Ujio wa ndege hizo unathibitisha kwamba Tanzania inaendelea kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira alisema kuwa Serikali ilifuatilia kwa karibu hatua zote za kutua kwa ndege ya KLM ikiwa ni pamoja na kuikaribisha ndege hiyo kwa maji kama ilivyo utaratibu. Aidha, kufika kwa abiria hao nchini kumesababishwa na imani ambayo Serikali imeijengea dunia.
“Tumeijengea dunia imani kwamba nchi yetu ni salama na ugonjwa wa Covid-19 uliopokuja tulipata na hofu na sasa tuimeishinda hofu na tumewasaidia na wao kuishinda hofu hiyo kwa kutojifungia ndani”, alisema Mgwira.
Aliongeza, “Katika kipindi hiki cha joto katika nchi zao kimewafanya waweze kuja kufurahia maajabu yaliyopo katika nchi yetu na kurudi na hii inatusaidia sisi kufanya biashara ya utalii ambapo leo tumepokea wageni 177 wote wakiwa watalii ambao watatembelea maeneo mbalimbali kwa siku kadhaa”
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa KIA, Christine Mwakatobe alisema kuwa kutua kwa ndege ya KLM nchini inadhihirisha namna ambavyo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) wameiona Tanzania ni sehemu salama.
Aidha, Mwkatobe alisema hatua hiyo ni muendelezo wa kuirejesha sekta ya utalii nchini ambayo iliathirika kwa kiasi kikubwa kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19.
“Baada ya shughuli za sekta ya utalii kurejea katika hali yake ya awali, sasa ajira nazo zimerejea, fursa mbalimbali za biashara na tunatarajia sekta hii itaendelea kuchangia pato kubwa katika Serikali”, alisema Mwakatobe
Hivi karibuni mashirika kadhaa ya ndege yakiwemo Qatar, Crystal, na Rwanda Air yamefanya safari zake nchini baada ya kuridhishwa na usalama wa abiria na pamoja na mali, huku hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 ikiwa shwari.