Profesa Gerald Misinzo (kulia) akitoa maelekezo kuhusu udhibiti wa panya kwa kutumia mkojo wa panya katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati wa Maoneshoya NaneNane, Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.
Mtaalam wa Maabara ya Udongo katika Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia (SUA), Stevenson Pelegy akitoa elimu ya jinsi ya kupima udongo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dutwa, mkoani Simiyu.
Baadhi ya Washiriki kutoka SUA katika Maonesho ya NaneNane mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja katika banda.
Na Mariam Mwayela, Simiyu
NAIBU Makamu Mkuu wa Utawala wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Maulid Walad Mwatawala amesema SUaina Mkakati wa kuhakikisha matokeo ya Tafiti zote zinazofanywa na watafiti zinawafikiakwa wakati.
Akizungumzia kuhusu maelekezo ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Maonesho ya NaneNane Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu Prof. Mwatawala alimesema kuwa SUA imeanzisha stashahada mpya ya Tejnolojia na Uzalishaji wa Mbegu (Diploma in Seed Technology and Production) ambayo ni maalumu kwa Maafisa Ugani ili kuwaongezea uwezo katika masuala ya mbegu.
“Stashahada hii itasaidia Mafisa Ugani kusambaza matokeo ya tafiti mbalimbali kwa wakulima ili kuweza kusaidia wakulima hao kulima kilimo chenye tija”, alisema Prof.Mwatawala.
Aidha aliongeza kuwa mbali na kuanzishwa kwa stashahada hiyo inayotarajiwa kuanza mwaka huu pia SUA imekuwa ikifanya mafunzo mbalimbali kuhusu mbegu kwa Maafisa ugani na wakulima kutoka katika Halmashauri na Taasisi mbalimbali nchini.
“Mpakasasa Halmashauri na Asasi au Taasisi za binafsi zimekuwa zikileta Maafisa Ugani na wakulima kwa ajili ya mafunzo mbalimbali juu ya ubebeshaji miche ya matunda na jinsi ya kusimamia kitalu cha miche na Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali kutokana na uhitaji na kwa sasa chuo kiko katika maandalizi ya kuandaa kalenda ya Mafunzo kwa mwaka mzima itakayokuwa inasambazwa kwa wadau mbalimbali ili kuweza kuja na kujifunza.” alisema Prof.Mwatawala.
Kuhusu suala la kutumia kilimo cha kunyunyiza na kuachana na Kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza gharama za kutengeneza miundombinu Prof. Mwatawala alisema SUA ina Shahada ya Masuala ya usimamiaji wa Rasilimali Maji hivyo kuna haja ya kuangalia ni namna gani watabadilisha ili kuweza kusaidia kutoka katika kilimo hicho cha umwagiliaji.
Mapema juzi mkoani Simiyu Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwaelekeza watafiti wa Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuhakikisha wanasambaza matokeo ya tafiti wanazofanya kwa Maafisa Ugani na wadau ili ziweze kuwafikia wakulima.
“Naelekeza watafiti watoe matokeo ya tafiti zao kwa maafisa Ugani ili ziweze kuwafikia wakulima na kunufaika na tafiti hizo,” alisema Mama Samia
Aidha ameiagiza Wizara ya Kilimo kutoa elimu ya utunzaji na uendeshaji endelevu wa miundombinu ya umwagiliaji hususan kujikita katika unyunyizaji na si umwagiliaji ili kupunguza gharama kubwa inayohitajika katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuelekeza kila mkoa, wilaya na Halmashauri kutekeleza agizo la kupanda miti na kuhakikisha inamea.
Chuo Kikuu cha Sokoine kinashiriki Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro na Kitaifa mkoani Simiyu ambapo Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo naUvuvi chagua Viongozi Bora 2020”.