…………………………………………………………………………………
Na Mbaraka Kambona, Tabora
Katika jitihada za kuboresha biashara ya mifugo na kukuza mapato ya ndani, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika bajeti ya mwaka 2020/ 2021 imetenga kiasi cha Milioni 681 kwa ajili ya kukarabati na kujenga minada ya mifugo nchini.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix Nandonde alipofanya ziara ya kukagua ukarabati unaoendelea kufanywa katika Mnada wa Ipuli uliopo Mkoani Tabora Mwishoni mwa Wiki.(Julai 30, 2020).
Akiongea baada ya kufanya ukaguzi huo alisema kuwa Wizara imetenga kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya kuboresha minada hiyo ili kuongeza tija katika biashara hiyo na kukuza mapato ya serikali.
“Serikali ya awamu ya tano imetenga kiasi cha shilingi milioni 681 kwa ajili ya kukarabati mnada huu wa Ipuli na Igunga hapa Tabora, pia itakarabati mnada wa Nata na kujenga mnada mpya wa kimkakati mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Wilaya ya Karagwe, eneo la Mulsagamba ili kuboresha biashara ya mifugo nchini,”alisema Dkt. Nandonde
Alisema ukarabati wa mnada wa Ipuli utagharimu kiasi cha shilingi milioni 92 na zinajumuisha ujenzi wa ukuta wa mnada, ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo, kipakilio cha mifugo na uboreshaji wa sehemu ya zizi.
Aliongeza kwa kusema kuwa ujenzi wa mnada wa kimkakati mpakani mwa Tanzania na Burundi utasaidia kutatua tatizo la muda mrefu la eneo la Tanzania kugeuzwa machungio na utafanya Tanzania kupata mapato kupitia mnada huo.
“Ujenzi wa mnada huu wa mpakani utaondosha tatizo la Wafanyabiashara wetu kudhulumiwa mitaji yao, lakini pia mnada huu utawavutia wafanyabiashara kutoka Burundi kuleta mifugo yao na hivyo kukuza pato la taifa kupitia biashara hiyo ya mifugo,”alifafanua Dkt. Nandonde
Awali akiongea kuhusu ukarabati wa Mnada wa Ipuli, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu alisema kuwa kuimarishwa kwa mnada huo kutasaidia kuongeza mapato kwa Halmashauri na Serikali, huku akisema kuwa ukarabati huo utazuia suala la utoroshaji wa mifugo katika eneo hilo.