………………………………………………………
Shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini limewajengea uwezo wachekechaji 60 wa madini ya Tanzanite wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara juu ya elimu ya afya na usalama.
Afisa miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise akizungumza kwenye kijiji cha Naisinyai amesema wachekechaji hao watapatiwa mafunzo hayo kwa muda wa siku mbili.
Mbise amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanachangia kupunguza athari za afya kwenye shughuli za uchekechaji.
Amesema pamoja na kutoa mafunzo hayo pia waliwapatia barakoa 400 kwa ajili ya kujikinga na vumbi wakati wakifanya shughuli zao za uchenjuaji mchanga wa madini ya Tanzanite.
“Pamoja na washiriki hao 60 pia kuna viongozi watano wakiwemo wa serikali hivyo kuwa na washiriki 65 ambao kwa namna moja au nyingine watakuwa mabalozi wazuri kwa wengine,” amesema Mbise.
Mwenyekiti wa wachekechaji wanawake wa Naisinyai, Nairukoki Leiyan amesema mashirika mengine yaige mfano wa Haki Madini katika kuwajali wadau wa madini ya Tanzanite.
Leiyan amesema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya shughuli zao ipasavyo na pia barakoa walizopatiwa zitawakinga na vumbi.
Mmoja kati ya wachekechaji hao Isaya Maliaki amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wa kufanya kazi zao kwa usalama zaidi tofauti na awali.
Maliaki amesema pamoja na mafunzo hayo pia barakoa waliopatiwa zitawakinga na vumbi wakati wakifanya shughuli zao za uchenjuaji mchanga wa madini ya Tanzanite.
Amesema wachekechaji hao wakitekeleza namna walivyofundishwa watakuwa salama kwani watakuwa wanashika michanga kwa kutumia vikinga mikono wakati wakifanya kazi zao.
Afisa afya wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Boniface Jacob amewapongeza Haki Madini kwa kuwajengea uwezo wachekechaji hao wa madini ya Tanzanite.
Jacob amesema zaidi ya kuwapa mafunzo ya kuwezeshwa kujikinga na vumbi pia barakoa waliopatiwa zitawakinga na vumbi na maambukizi ya virusi vya corona kwani wanapaswa kuendelea kujikinga.
MWISHO.
Ofisa miradi wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini, Emmanuel Mbise akizungumza na wachekechaji wa madini ya Tanzanite wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwenye mafunzo ya siku mbili ya elimu ya afya na usalama kwa wachekechaji.