*****************************************
25,July
Na MWAMVUA MWINYI,PWANI
RANCHI ya Ruvu ,Bagamoyo mkoani Pwani ni moja ya Ranchi zilizokuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi baina yake na wananchi ,uvamizi wizi wa mifugo ya Ranchi na ufugaji holela hali ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo changamoto hizo zinaelekea kuwa historia.
Hii hali ilisababishwa na tatizo la kutokuwa na mipaka na alama zinazoonyesha eneo la Ranchi ambapo baada ya kuwekwa alama hizo tatizo la migogoro hiyo limepungua .
Katika hatua nyingine ,wamefanikiwa kuokoa kiasi cha sh .milioni 20 zilizotokana na upunguzaji wa watumishi wasio wa lazima ,kujenga miundombinu imara isiyoongeza gharama za kiutendaji na kupunguza matumizi yasiyo ya ulazima.
Kauli hivyo imetolewa na meneja wa Ranchi ya Ruvu, Elisa Binamungu ,alipokuwa anaelezea mafanikio ,maboresho na changamoto za Ranchi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1957.
Anasema miaka mitano iliyopita kulikuwa na kero ya migongano na jamii kuingilia Ranchi ,wizi wa mifugo ya Ranchi, kwa kuweka alama za kudumu kutenganisha maeneo ya Ranchi na jamii kumesaidia kupunguza migogoro ya ardhi sanjali na kutenga eneo la hekta 20,000 ambalo limepimwa vipande vya hekta 500 na kupatikana vitalu 40 vinavyotumika kwa wafugaji wadogo ili kupunguza pia mifugo holela mkoani hapo .
Anaeleza ,wanahamasisha kuanzia ngazi ya kijiji ,kata lengo mifugo inayoingia ndani ya Ranchi iingie kwa utaratibu maalum ikiwa ni pamoja na kila heka moja mfugaji anailipia 5,500 kama tozo kwa mwaka .
“Tozo hii kwasasa imeshuka kutoka 5,500 hadi 3,500 baada ya wafugaji kulalamikia tozo ni kubwa kwa mwaka”
Binamungu anasema ,upande wa mapato umeongezeka kutoka milioni 50 kwa mwezi hadi kufikia makusanyo ya milioni 100 ..
“Fedha hii imeongezeka lutokana na mauzo ya nyama ,ngozi ,tozo za vitalu na wanyama wadogo ” anasema Binamungu .
Anaelezea kwamba ,nyama wanauza ya kiwango ,kilo moja 7,000 ,wana duka la nyama katika Ranchi na jingine Dar es salaam ,wanauza kwa wateja mmoja mmoja ,jumla na kwa wasambazaji kwa wenye mahitaji .
Binamungu alitaja malengo yao kuwa ni kuboresha miundombinu zaidi ili kujiimarisha ,kujenga machinjio ya kisasa .
Lengo jingine ni kuongeza uzalishaji wa mifugo ya maziwa kwani wamegundua kuna fursa kubwa ya uuzaji maziwa baada ya soko kupanda la maziwa huku kukiwa na upungufu wa maziwa .
Tunahitaji kuanzisha mashamba darasa ,hii ni Ranchi kubwa mashamba darasa yatasaidia kuwaongezea ulewa wafugaji kufuga na kuondokana na uchungaji ,wa kufuga kiholela ,kienyeji ,ni wajibu wao kufuga kisasa .
Meneja huyo wa Ranchi ya Ruvu ,anatoa rai kwa wafugaji kuachana na uchungaji uliopitwa na wakati na badala yake wafuge kisasa kwa kuwapa lishe bora mifugo na tiba sahihi .
Binamungu anatoa wito kwa wafugaji kujiunga vikundi vidogo ili kuomba maeneo katika Ranchi hiyo ili pia kupunguza migogoro na wakulima kwenye maeneo yao .
Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa anatoa onyo kwa baadhi ya viongozi wa vijiji na watendaji wanaoshiriki kukaribisha wafugaji bila utaratibu na waache mara moja ,kwani ndio kichocheo cha uvunjifu wa amani na migogoro baina yao na wakulima .
Ranchi ya Ruvu ,ilianza mwaka 1957, kwasasa ina jumla ya wafanyakazi 43, mifugo ya ng’ombe 1,500 ,mbuzi 400 na kondoo 780.