Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi wakiwa kwenye kikao cha kupitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali leo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye akijadiliana jambo na Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo bi Halima Mpita wakati kikao kikiendelea.
**************
Na Danny Tweve –Songwe
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mbozi limeazimia kuchukua hatua za kuwekeana makubaliano na bodi ya Kahawa nchini TCB ya lini madeni ya muda mrefu yatalipwa baada ya Bodi hiyo kutowasilisha fedha zote za mwaka 2016/2017 ambazo ilizikusanya kama wakala wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwenye ushuru wa Kahawa.
Wakichangia kwenye kikao cha kupitia taarifa ya Mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali, wajumbe wa baraza hilo wameonyesha hofu yao kutokana na Bodi ya Kahawa kulipa kiasi cha Tshs 264,770,394.39 kati ya Tshs 602 Milion ambazo halmashauri hiyo inazidai kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa bodi hiyo.
Wakijadili hoja juu ya wadaiwa wa Halmashauri, ambapo inaonyesha Mbozi inawadai taasisi, mashirika na watu binafsi kiasi cha shilingi 856,164,498 na kati ya hizo kwenye ukaguzi huo, Tshs 612,612,612 sawa na asilimia 72 ni madeni ya muda wa miezi 12 wakati kiasi cha zaidi ya 242 Milioni(28%) ni madeni ya muda zaidi ya miezi 12.
Kutokana na hali hiyo diwani wa Ipunga Burton Sinienga alitaka kupata ufafanuzi lini taarifa ya ukaguzi maalumu ya TCB itawasilishwa kwenye baraza hilo ili kuondoa utata wa kiwango ambacho halmashauri hiyo inaidai bodi ya kahawa kutokana na halmashauri kudai Tshs 603 Milion wakati bodi inakiri kudaiwa kiasi cha shilingi 440 milion.
Kwa upande wake diwani wa Halungu Maarifa Mwashitete ameomba msukumo wa mkoa kusimamia makubaliano baina ya Bodi ya Kahawa na Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kutokana na deni hilo kuchukua muda mrefu bila kulipwa hali ambayo inakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.