Mgombea urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi (kwenye gari mbele) akiwapungia mkono wananchi na wana-CCM waliojitokeza katika mapokezi njiani. |
Na Mwandishi Wetu, Pemba
MGOMBEA nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi amepata mapokezi makubwa alipowasili Kisiwani Pemba kwa ajili ya kutoa shukrani kwa kuaminiwa.
Mapokezi makubwa ya mgombea huyo yalianzia katika Uwanja wa Ndege wa Karume, Mkoa wa Kusini Pemba na kupita Barabara Kuu kuelekea Viwanja vya Tibirinzi akiwa katika gari la wazi, huku akisindikizwa na umati wa watu wenye sare za CCM na wengine wakimpungia mikono kando ya barabara.
Katika viwanja vya Tibirinzi, Chakechake, Kusini Pemba, vilifurika watu hadi mamia ya wananchi wakijikuta wamekosa nafasi ndani ya uwanja huo na kubaki nje ya viwanja hivyo wakiendeleza shamrashamra za mapokezi.
Akizungumza na wananchi, Dk. Hussein Mwinyi alianza kwa kukishukuru chama chake kwa kumaliza uteuzi kwa haki jambo ambalo limefanya waliokuwa wakiomba ridhaa pamoja naye sasa kuungana na kuwa kitu kimoja kuhakikisha CCM inashinda na kuchukua dola.
“…Nashukuru chama kwa kumaliza uteuzi wake kwa kwa haki, na sasa sote tumekua wamoja, hakuna timu Mwinyi wala timu Mbarawa, na lengo letu sasa ni moja kushika dola,” alisema.
Dk. Hussein Mwinyi aliwahakikishia wananchi kuwa akifanikiwa kushinda atahakikisha anaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964, pamoja na kudumisha Muungano.
Alisema suala kubwa akifanikiwa kuingia Ikulu ya Zanzibar ni kudumisha amani ili kuchochea maendeleo. Nchi nyingi za jirani hakuna amani jambo ambalo linakwamiasha suala la maendeleo.
“…Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuongoza nchi kwa amani. Jukumu langu ni kuhakikisha amani inadumu. Lazima tudumishe umoja wetu. Kusiwe na Upemba na Uunguja, kusiwe na ukusini na Ukaskazini. Sote ni Wazanzibari,” alisema Dk. Mwinyi.
Aidha aliongeza kuwa akiingia madarakani suala la ajira atahakikisha analishughulikia hasa kwa vijana, huku akimpongeza Rais Dk. Shein na viongozi wote wa Serikali na chama wanaomaliza muda wao kwa kufanya vizuri, jambo ambalo linamfanya aendeleze walipoishia.
“Nitaendeleza miundombinu, huduma za jamii, ustawi wa watu, maendeleo ya jamii, afya, elimu, na yote yanayogusa watu. Nitahakikisha Mzazibari anakua na maisha bora. Ukitaka kuyafanya hayo, lazima uwajibike. Huwezi kuwa na program kukawa na wala rushwa, wabadhirifu, Wazembe,” alisema mgombea huyo.
Alibainisha kuwa Serikali yake itafanya kazi kwa maslahi ya Wazanzibari wote bila ubaguzi. Aliwatoa hofu wanaosema yeye ni mpole katika utendaji, kwamba hiyo si kweli bali ni kutokana na nafasi yake ya Waziri wa Wizara ya Ulinzi sehemu ambayo mambo mengi ni ya siri kiutendaji.
“…Nasema haya kwa sababu pengine hamjanisikia nikiongea sana kwenye vyombo vya habari. Sababu kubwa ni kwamba Wizara ya Ulinzi huko mambo yetu ni ya siri hatufanyi hadharani. Siwezi kusema ila kwa wale wabadhirifu, wala rushwa, wazembe, wasiowajibika, hao watawajibika,” alisisitiza Dk. Mwinyi.
Aliahidi kusimamia maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya za Kimataifa. Dhamira yake ni moja tu ya kuwatumikia Wazanzibari wote bila kubagua endapoatafanikiwa kushinda.
“Mwaka huu, tunataka tupate ushindi wa kishindo usiwe mwembemba tukapata malalamiko. Na niliyoyaona Unguja na hapa Pemba kwa sasa sina
ushindi ni mkubwa. Sina shaka ushindi utakua ni mkubwa. Nasema tena kwamba ‘Yajayo yanafurahisha.’ Ni ahadi naichukua mbele ya Mungu na mbele yenu. Nitahakikisha nawahudumia wananchi.”
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi (kwenye gari ) akionesha ishara ya kuwashukiuru wananchi waliojitokeza njiani kumpokea. |