……………………………………………………………………………
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, inamshikilia Ofisa uchumi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Colman Urasa kwa tuhuma za kudaiwa kugawa maeneo ya kujenga vibanda katika uwanja wa Kwaraa uliopo mjini Babati.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari amesema Urasa aligawa viwanja hivyo kwa kugawa kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja hivyo kuzua sintofahamu miongoni mwa wana Babati.
Makungu amesema halmashauri ya mji huo ilitoa eneo maarufu linalofahamika kama uwanja wa Kwaraa uliopo katikati ya mji wa Babati ili wenye uhitaji wa kujenga majengo kwa ajili ya biashara wafanye hivyo kulingana na mikataba waliyokubaliana.
“Hata hivyo ili ujenzi usiwe holela, halmashauri imepeleka katika eneo hilo wataalamu kwa ajili ya kusimamia upimaji, ugawaji na ujenzi wa eneo hilo,” amesema Makungu.
Amesema uchunguzi wao unaonyesha kuwa Urasa ambaye amepewa wajibu wa kusimamia upimaji na ugawaji wa maeneo hayo amekuwa akigawa maeneo hayo kwa wananchi waliotimiza masharti kama yaliyoainishwa na Halmashauri.
Amesema hata hivyo baadhi ya wananchi wanapoleta mafundi wao kwa ajili ya kuanza ujenzi hukuta eneo alilokuwa amegawiwa likiwa amepewa mtu mwingine ameanza ujenzi.
“Hali hiyo inayopelekea sintofahamu kati ya wananchi na kuona halmashauri kama inawatapeli, ifahamike kwamba alichofanya Urasa ni kosa la matumizi mabaya ya madaraka chini ya k/f cha 96 cha kanuni ya adhabu,” amesema Makungu.
Amesema wanaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na mara utakapokamilika sheria itachukua mkondo wake, wanawaomba wadau wote waliokumbana na adha ya maeneo waliyopangiwa kupewa watu wengine wafike ofisi za TAKUKURU Babati Julai 13 mwaka huu ili tuhuma dhidi ya Urasa zishughulikiwe kwa ujumla wake.