Meneja wa chama cha ushirika cha Msingi Kimuli Ernest Komba akionyesha baadhi ya miradi wanayoitekeleza katika chama chao wajumbe wa chama kikuu cha Ushirika cha Mbifacu hivi karibuni walipotembelea chama hicho kukaguua miradi ya Maendeleo..
……………………………………………………………………………..
Chama cha Ushirika cha msingi kimuli, ambacho kipo, katika Kijiji cha Utiri, kata ya Utiri Wilayani Mbinga, kimetoa shilingi milioni mia moja (1000,000,000/=), kwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Kitanda, Utiri na Kihangi mahuka Wilayani hapa.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Chama hicho Bw Ernest Komba, wakati akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Chama hicho, Katika Ziara ya kukagua Shughuli za Chama hicho cha Msingi iliyofanywa na Viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika Mbinga (Mbifacu), hivi karibuni Wilayani hapa.
Bw Komba alifafanua kuwa fedha hizo zimetolewa na Chama cha kimuli, zilitokana na mapato ya premium na ziada, za Ndani na kusaidia ukarabati wa majengo ya Taasisi za elimu na Afya, zilizomo katika maeneo yanayohudumiwa na Chama cha kimuli.
Aliitaja miradi aliyoipa fedha hizo kuwa ni Zahanati ya Lipumba (14,000,000/=) ,Zahanati ya Kitanda (9,5000,000/=), Zahanati ya Utiri (7,000,000/=) na Sekondari ya Ndela (15,000,000/=). Miradi mingine ni Sekondari ya Kihangi Mahuka (13,000,000/=), Sekondari ya Luli (2,500,000/=), Sekondari ya Ngwilizi (13,000,000/=) ,na Shule za Msingi 10 zilizoko katika Kata ya Utiri na Kitanda, ambazo zimepewa tsh (26,000,000/=).
Awali wananchi walikuwa wakichangia fedha za mifukoni, au kusubiri miradi itekelezwe na Serikali. Lakini kwa sasa Chama kimeona kisaidia kufanya maendeleo hayo ili kurudisha fadhila kwa wananchi ambao huuza mazao katika chama cha msingi na wananchi waone faida ya uwepo wa chama cha Ushirika na Msingi Kimuli.
“Chama kimetoa faida yake kwa kuchangia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ya Afya na elimu kwa kuchangia ukarabati na ujenzi wa madarasa kutokana na uhitaji wa taasisi husika, ili kuamsha ari kwa jamii na watambue umuhimu wa chama chao cha Ushirika, kwa kuwa kama sio chama kutoa kiasi hicho basi wangelazimima kuchangia au kusubiri Serikali itoe Fedha za kutekeleza miradi hiyo ya Maendeleo”. Alisema Komba
Alitoa wito kwa Wananchi wa kata zilizo katika mradi, huo wajiunge na Chama cha ushirika na Msingi Kimuli kwa Maendeleo ya kaya na Jamii kwa ujumla kwa kuwa mbali na Utekelezaji wa Miradi hiyo, huduma zingine zinazotolewa ni mradi wa Mashine ya kusaga nafaka ambao hutoa huduma kwa wanachama, lengo likiwa ni kupata uzoefu na kupata uzoefu wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata unga wa mahindi. kwa sasa chama kina mashine tatu katika Vijiji vya Utiri Mtama na Kitanda.
Kaimu Mganga kiongozi wa Zahanati ya Utiri, Bi Marietha Ndunguru, alisema anawapongeza sana Chama cha Ushirika Kimuli kwa kuwasaidia misaada mbalimbali ikiwa nia pamoja na Bati,vifaa vya kunawia na kujikinga na Corona lakini hata sare za hizi tulizovaa tulipata msaada toka Kimuli.Tunashirikiana nao vizuri.
Aliitaja Miradi mingine kuwa ni Mradi wa Mashamba ya miti ambapo mpaka sasa tayari wameshapanda ekari 30 za miti katika kijiji cha Kitanda, mahande na Mtama lengo likiwa ni kuwa ni kitega uchumi kitakachoongeza mapato katika chama hicho hapo baadaye.
Mradi mwingine ni Chama kimekuza miche bora ya kahawa ili kukuza hali ya uzalishaji wa zao hilo.Katika Msimu huu Chama kinaendelea kukuza miche 120,000 ambayo kwa sasa imeoteshwa kitaluni na kuwauzia wakulima kwa bei rahisi ili wakulima waweze kuzalisha Kahawa bora.Pia chama kina mradi wa usafirishaji mizigo kwa kutumia magari ya Chama kwa lengo la kusafirisha mbolea,kahawa na vifaa vya ujenzi, ili kuongeza pato la Chama.
Aidha Mradi mwingine ni Mradi wa mazao,Chama hukusanya Mazao ya wanachama na ya wakulima wengine kuyachakata na kuyatafutia soko.Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuviongezea nguvu vyama vya Ushirika na Msingi kwa kuwa kwa sasa wakulima wengi mara baada ya kupata Elimu ya Ushirika wanauza mazao yao kupitia vyama vya ushirika na kupata manufaa mengi ikiwemo kusomesha watoto kunua pembejeo na kukuza pato la familia.
Kwa upande wake Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Ruvuma Bi bumi Masuba alikipongeza chama kikuu cha Mbinga kwa kusimamia vema Vyama vya Msingi vinavyoisimamia kwa kuwa vyote vinakwenda vizuri na Vinapata mafanikio na kutoa wito kwa wananchi kuvitumia Vyama vya Ushirika na Msingi vilivyoko katika Maeneo yao.