NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ametoa rai kwa wakandarasi katika wilaya mbalimbali kuongeza kasi ili kuhakikisha wananchi wanapata nishati vijijini ,kama ilivyo maagizo ya Rais Dk.John Magufuli mpaka 2021 vijiji vyote kuunganishiwa umeme .
Aidha ametoa rai kwa wanyakazi wa TANESCO katika Ofisi za Wilaya nchi nzima, hususan kada ya maofisa uhusiano na huduma kwa wateja, kufanya kazi kwa kujituma kwa kutoka maofisini kwenda kutafuta wateja ili kuliongezea shirika mapato.
Alisema hayo wakati akiwasha rasmi umeme kijijini hapo kwenye duka la Abdul Abdulrahman, ikiwa ni ishara ya kukiwashia kijiji kizima.
Subira alieleza, mikakati ya serikali kufikisha umeme katika maeneo yote nchini.
Alisema kuwa ,matarajio ni kuvifikishia nishati hiyo vijiji 10,268 nchi nzima ifikapo Juni 2020, vikiwemo vijiji vipya 60 vya Wilaya ya Mkuranga.
Akizungumzia uwajibikaji kwa wafanyakazi wa TANESCO Subira,alisema hasa kada ya maofisa uhusiano na huduma kwa wateja, ijitume, kuhakikisha wanawafuata wateja mahala waliko kwa ajili ya kuwapelekea taarifa mbalimbali pamoja na kupokea kero zao.