Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Kashilimu Mayunga kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa mtandao wa maji katika mradi wa Ntomoko uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Kazi ya uchimbaji mtaro kwa ajili ya kubadilisha mabomba yaliyochakaa ikiendelea katika mradi wa maji wa Ntomoko.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) David Palangyo akitoa maelezo ya mradi wa Ntomoko.
………………….
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) jana alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Ntomoko uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba jijini Dodoma.
Waziri Mbarawa amesema mradi wa Ntomoko ulikuwa na changamoto kubwa za ubadhilifu iliyopelekea baadhi ya watu kupelekwa katika vyombo vya sheria.
Aidha, serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ilisaini mkataba tarehe 11 Februari, 2019 na China Railway Seventh Group (CRSG) kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mradi wa maji wa Ntomoko ikiwa ni hatua mahususi ya kumaliza changamoto ya mradi huo ili wananchi waweze kupata majisafi na salama.
“Wizara itahakikisha malipo ya Mkandarasi yanafanyika kwa wakati na nyie mliopewa dhamana ya kusimamia hakikisheni mkandarasi anafanya kazi kufuatana na maelekezo yaliyopo katika mkataba, ni muhimu sana vinginevyo anaweza kufanya kazi isiyokuwa na viwango vinavyokubalika”, alisema Profesa Mbarawa.
“Hakikisheni mkandarasi anamaliza kazi kwa muda mfupi badala ya mwaka mmoja, wananchi hawawezi kuendelea kupata shida ya maji”.
Akitoa maelezo ya mradi kwa Mhe. Waziri wa Maji, Meneja Ufundi Mhandisi Kashilimu Mayunga alisema thamani ya mkataba wa ukarabati wa mradi wa maji Ntomoko ikijumuisha fedha za ujenzi, ukarabati pamoja na usimamizi wa mradi ni shilingi 2,269,376,877.75.
Mhandisi Kashilimu amesema malipo ya awali ya shilingili 680,813,063.33 yameshafanyika na Mkandarasi amesha anza kazi rasmi tarehe 07 Juni, 2019.
Utekelezaji wa mradi huu unatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 12 na unatarajiwa kunufaisha jumla ya wakazi wapatao 20,736 sawa na Kaya 5,184 ambapo katika awamu hii mradi unalenga kufikisha huduma katika vijiji vinne (4) viwili vya Makirinya na Ntomoko vilivyopo Halmashauri ya Kondoa na vijiji vya Lusangi na Kinkima viliyopo Halmshauri ya Wilaya ya Chemba.