********************************
Na Grace Michael, Dar es Salaam
WANANCHI wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa kuanzisha mpango wa vifurushi ambavyo vinatoa fursa kwa kila mwananchi kujiunga na huduma zake na kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.
Hayo wameyasema leo katika banda la NHIF kwenye maonesho ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere walipofika kwa ajili ya kupata elimu ya bima ya afya.
“Kuanzishwa kwa mpango huu ni ukombozi mkubwa kwetu wananchi ambao awali hatukuwa na nafasi ama fursa ya kujiunga na huduma hizi, tuliziona huduma hizi kwa watu wachache lakini sasa hakuna aliyeachwa nje ya Mfumo tunawapongeza sana na endeleeni kuwafikia wananchi na kutoa elimu tu,” alisema Mkazi wa Buguruni Ally Rashid.
Alisema kuwa kutokana na utaratibu uliokuwepo zamani, wananchi wengi waliachwa nje ya Mfumo hivyo kurahisishwa kwa utaratibu wa kujiunga kumetoa wigo mpana kwa wananchi kufanya uamuzi wa kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya.
Naye mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam Bw. Jackson Nguma alisema kuwa huduma za matibabu ni huduma za msingi kwa kila mwananchi hususan katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na maradhi mengi ikilinganishwa na zamani lakini pia kuwepo kwa gharama kubwa za matibabu hivyo kuwepo kwa NHIF ni mkombozi wa huduma za matibabu kwa wananchi.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Helena Nzaliwa mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, alisema kuwa huduma za matibabu ni mahitaji ya msingi ndani ya familia yoyote kutokana na ukweli kwamba familia inapokuwa na mgonjwa haiwezi kufanya kazi yoyote ya kimaendeleo hivyo kitendo cha kuwa ndani ya bima ya afya inaleta kujiamini kwa familia husika.
“Kwanza nawapongeza sana NHIF kuwepo katika maonesho haya na kwenye maeneo mbalimbali wanayofika, bima ya afya inahitajika sana kwa kila mwananchi ili kuondokana na hofu ya kukosa matibabu pale anapopatwa na magonjwa, niwaombe wananchi wenzangu kutumia fursa hii kufika katika banda la NHIF ili kujiunga,” alisema Bi. Nzaliwa.
Huduma za elimu na usajili zitaendelea katika banda la NHIF lililopo nyuma ya banda la Jakaya Kikwete mpaka tarehe 13 Julai, 2020.