………………………………………………………………….
NA MWAMUA MWINYI,VIGWAZA
DIWANI anaemaliza muda wake kata ya Vigwaza,Chalinze,Mohsin Bharwani ametoa rai kwa wananchi wa kata hiyo waendelee kukiamini chama cha Mapinduzi kwa kuichagua CCM pamoja na kuchagua diwani na mbunge mwenye kasi inayoendana na Rais Magufuli ambao watasimama kidete kupigania kuondoa vilio na kero zao ili kuinua maendeleo zaidi.
Aidha amewasihi vijana lithubutu na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo na kuacha kuogopa kwani ni haki yao ya msingi.
Mohsin alitoa rai hiyo,wakati akiwaaga rasmi wananchi wa Ruvu Darajani na Kidogozero ,kata ya Vigwaza ,kuwa anamaliza muda wake mahala salama kimaendeleo hivyo ni wakati wa kuchagua diwani atakaeendeleza maendeleo hayo kwa kasi zaidi ili kutatua kero zao.
Alisema katika uongozi wake ametumia zaidi ya sh.milioni 171 na kujitolea misaada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau na wafadhili na fedha ake mfukoni kuchangia miradi mbalimbali na kusaidia makundi maalum.
Mohsin alieleza kwamba,wakati tukiwa tumeingia katika uchumi wa kati wananchi wanahitaji viongozi wanaofaa kuwavusha pale walipo sasa,kusimamia shida zao badala ya kuendekeza siasa,propaganda zisizosaidia jamii.
“Ninaondoka,ila sitowaacha pale mtakaponihitaji kuchangia shughuli za kimaendeleo,naondoka katika udiwani lakini kwenye siasa bado nipo”
‘”Nawashukuru wananchi,vingozi wenzangu kuanzia shina,matawi,kata,na wilaya na mkoa katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi,nawashukuru mabalozi ambao wote mlionisaidia kufikisha Vigwaza ilipofika”alifafanua Mohsin.
Hata hivyo Mohsin alitoa kiasi cha sh.500,000 kusaidia kikundi cha wazee na kuchangia mtofali 1,000 na mifuko ya saruji 50 ikiwa ni kuunga mkono ujenzi wa madarasa manne katika shule ya msingi Ruvu Darajani.
Awali mtendaji wa kata ya Vigwaza Ali Mzuri Hamis akisoma taarifa ya utekelezaji ya kata wakati wa uongozi wa diwani huyo anaemaliza muda wake,alisema aliweza kuchangia matawi milioni 7.5,alichangia dawa za binadamu zahanati Vigwaza na Ruvu Darajani zenye thamani ya milioni 4.5.
Alichangia pia shule kumi za msingi na sekondari vifaa mbalimbali milioni 6.4,amesaidia wananchi mbalimbali na makundi maalum milioni 25,pia alitoa mchango kwa wanafunzi shule 11 mabati,saruji na kukarabati milioni 38.7 na kusaidia sadaka na chakula katika kaya maskini milioni 13.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Vigwaza ,Shedeli Mikole alimshukuru Mohsin kwa kuiacha CCM pazuri na kuweza kumsemea kwani angekuwa diwani ambae hajatekeleza wala kuwa karibu na jamii wasingejua wanaanzia wapi.
Alisema,ni viongozi wachache wanaoweza kuchaguliwa na kujitoa kama alivyo yeye na kusema wataendelea kumtumia ili kuimarisha chama na kusaidia kuchagua miradi ya wananchi.
Baadhi ya wananchi kata ya Vigwaza wamesononeka kuaga kwa diwani huyo na kutangaza kutogombea uchaguzi mkuu ujao,na kusema wanaombea waweze kuchagua na kupata diwani atakaemzidi Mohsin na kusukuma maendeleo kama alivyokuwa .
Mwisho