Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa mkoa wa Kigoma waliojitokeza kushuhudia uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma jana.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma uliofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua moja ya majalada la ardhi katika ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma alipokwenda kuizindua rasmi. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga na wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Kigoma Chediel Mrutu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi hati ya ardhi mmoja wa wananchi wa mkoa wa Kigoma wakati wa uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoani humo jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa mkoa wa Kigoma waliokabidhiwa hati za ardhi wakati wa uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoani humo jana. Wa nne kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza mkazi wa Kigoma aliyewasilisha malalamiko kwake wakati wa uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoani humo jana. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
******************************
Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Maafisa Mipango Miji nchini kuzisaidia wilaya kuhakikisha maeneo yote ya vijiji yanayochipukia kuwa miji anapelekewa ili ayatangaze kuwa maeneo ya Mipango Miji.
Lukuvi alisema hayo jana wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini. Tayari ofisi za ardhi kwenye mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi zimezinduliwa.
Alisema, wizara yake kwa sasa ina mpango wa kupima kila kipande cha ardhi nchi nzima sambamba na kuhakikisha maeneo yanapangwa ili kuepuka ujenzi holela.
‘’Maeneo yote ambayo vijiji vinachipukia nileteeni nitangaze kuwa maeneo ya mipango miji na maafisa mipango miji mzisaidie wilaya katika hili’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, baada ya maeneo hayo ya vijiji vinavyochipukia kutangazwa maeneo ya mipango miji wananchi wake hawatapewa tena hati za kimila na badala yake watapata hati za miaka 99 kama wanavyopata watu wanaoishi mijini.
Alisema, mpango wa kuyatangaza maeneo hayo ya vijiji inavyochipukia siyo lazima uanzie wizarani bali Maafisa Mipango Miji katika halmashauri za wilaya wanatakiwa kuyawahi mapema ili kuepuka ujenzi holela.
Akizungumzia utendaji kazi katika ofisi za ardhi za mikoa, Waziri Lukuvi alisema, ofisi hizo zimekamilikia kutokana na kuwa na wataalamu wa fani zote kama vile Upimaji, Uthamini, Mipango Miji pamoja na Usaji wa Hati na kubainisha kuwa vifaa vya kisasa vya upimaji navyo vimepelekwa kwenye ofisi hizo na sasa mwananchi halazimiki kufika Wizarani kwa kuwa huduma zote zinapatikana ofisi za mikoa.
Kuhusu upungufu wa watumishi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri za wilaya, Lukuvi alisema kuwa, baada ya kupeleka watumishi ngazi ya mkoa, zoezi linalofuata ni kuwapanga upya watumishi katika ngazi ya halmashauri kwa kuzingatia wataalam wa fani zote.
Akigeukia suala la utoaji hati miliki za ardhi nchini, Lukuvi ameagiza wananchi wote waliopimiwa ardhi kwenye mkoa wa Kigoma kwenda ofisi za halmashauri za wilaya kuomba kutengenezewa hati na kubainisha kuwa, atakayeshindwa baada ya siku tisini atapelekewa hati ya malipo na kudaiwa kuanzia tarehe aliyopimiwa kiwanja chake.
‘’kama hukwenda kujisalimisha kudai hati ya eneo lako lililowekewa mawe basi baada ya siku tisini utaletewa bili na utadaiwa kuanzia siku ambayo kiwanja chako kiliwekewa mawe, kama yaliwekwa mwaka 1986 basi utaanza kudaiwa kuanzia hapo’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma Chediel Mrutu, mkoa huo una wamiliki wa viwanja 14,746 ambao hawajachukua hati zao pamoja na kukamilika taratibu zote za umilikishwaji ikiwemo kuwekewa alama jambo linaloikosesha serikali mapato sambamba na wamiliki wake kukosa fursa za kiuchumi zinazotokana na kuwa na hati miliki
‘’Usipokuwa na hati ya kiwanja hukopesheki, ongezeni thamani ya mitaji yenu na ardhi isiyopimwa inaitwa mitaji mifu na unapopima ardhi yako na kumilikishwa unakuwa na kinga ya kisheria ‘’ alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliielezea ardhi kama msingi wa haki na dhuluma yoyote inayofanyika inaweza kuleta vita kwa kuwa ardhi ina rasilimali mbalimbali. Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga, uanziushwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Kigoma utawezesha wana kigoma kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo kusafiri hadi Tabora kuifuta huduma kwenye ofisi ya kanda.
Mapema Kamishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu na Usimamizi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa unaenda sambamba na usambazaji vifaa vya kisasa kwenye ofisi hizo ili kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikshaji ambapo alibainisha kuwa ardhi inaweza kutumika kama sehemu ya mwananchi kujiongezea kipato.