Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi akizungumza na watumishi wa ofisi yake wanaotarajia kustaafu hivi karibuni wakati wa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma.Mafunzo hayo yalifanyika Juni 21, 2019 Jijini Dodoma.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Bi. Ziada Sadick akizungumza jambo kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaotarajia kustaafu hivi karibuni wakati wa mafunzo ya ya maandalizi ya kustaafu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi akimkabidhi cheti cha mafunzo ya maandalizi ya kustaafu Mtunza Kumbukumbu Mkuu wa ofisi hiyo Bi. Amina Simbaulanga ambaye anatarajia kustaafu mwezi mwishoni mwa mwaka huu.
………………….
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Bi.Maimuna Tarishi amewaasa watumishi wa Ofisi hiyo wanaotarajia kustaafu hivi karibuni kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi hadi siku zao za kuhitimisha utumishi wao katika Ofisi hiyo zitakapofika.
Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kujiandaa kustaafu yaliyoandaliwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea aliwaeleza umuhimu wa kuendelea kuwajibika kulingana na taratibu na kanuni zinazoongoza utendaji kazi wa kika siku.
“ Hatutarajii kuona kati yenu hata mmoja wenu akianza kuchelewa kazini au kuanza kuzembea katika kutekeleza majukumu yake kwa kuwa anatarajia kustaafu mwaka huu, tunatarajia kuwa sasa mtaendelea kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuwarithisha utamaduni wa kupenda kufanya kazi kwa bidii wale wanaobaki” Alisisitiza Bi Maimuna
Akifafanua amesema kila mtumishi wa umma anayetarajia kustaafu anapaswa kuhakikisha kuwa anaendelea kuonesha mfano bora katika sehemu yake ya kazi kwa kutekeleza yale anayotakiwa kwa weledi na kwa wakati akizingatia maslahi ya nchi.
Aliwaasa watumishi hao kutumia vizuri elimu waliyopatiwa kupitia mafunzo yakuwaandaa kustaafu yaliyoandaliwa na Ofisi hiyo ili hatimaye wanapostaafu waweze kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni Bi. Ziada Sadick amesema kuwa Chuo hicho kinaipongeza Ofisi yan Waziri mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo kwa watumishi wake wanaotarajia kustaafu hivi karibuni.
Aliongeza kuwa mafunzo haya yanawapa uwezo watumishi hao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza zikawakabili baada ya kustaafu.
Katika mafunzo hayo watumishi wanaotarajia kustaafu waliweza kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuanzisha miradi ya uzalishaji, mbinu za kukabilina na msongo wa mawazo na mada nyingine mbalimbali.Mafunzo hayo yalishirikisha watumishi takribani ishirini wa kada mbalimbali.